Skip to main content
Habari na Matukio

Kuongezeka kwa Bei ya Bidhaa za Nafaka ni Furusa kwa Wakulima

Kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula kama mchele na mahindi mijini kwa kiasi kikubwa kumechangiwa  na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa hizo katika nchi jirani.

Hayo yamesemwa na waziri wa Kilimo chakula na ushirika Mh.Christopher Chiza alipokuwa anaongea na waandishi wa habari katika uwanja wa Mnazi mmoja hivi karibuni
Chakula kutoka Tanzania kimekuwa kikisafirishwa katika nchi za Sudani, Somalia na baadhi nchi jirani hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji ya chakula na kufanya bei yake kuwa juu.

Aidha,  bei ya mchele mijini hususan katika jiji la Dar es Salaam imefikia shilingi 2,300 kwa kilo. Pamoja na jitihada za kuingiza mchele kutoka nje, bei yake na hata mahindi haijashuka. Hii ni ishara ya mahitaji makubwa ya nafaka (hasa mchele na mahindi) katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Pembe ya Afrika.

Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kutoka katika nchi za jirani, wakulima na wadau wa kilimo nchini Tanzania wametakiwa kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji kwa kuwa kuna uhakika wa soko la mazao hayo.

Wizara ya Kilimo chakula na Ushirika na wadau wake imeanzisha  mkakati wa kuendeleza zao la mpunga (National Rice Development Strategy – NRDS) ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo mara dufu ifikapo 2018. 

Mkakati wa Kupambana na Changamoto za Zao la Mpunga

Waziri wa kilimo chakula na ushirika Mh. Eng. Christopher Chiza ametaja upatikanaji mdogo wa mbegu bora kama mojawapo ya changamoto inayokumba zao la mpunga, wakati akiwahutubia wakulima na wadau wa zao hilo ambao walihudhuria maonyesho ya zao la mpunga yaliofanuyika katika uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam yaliyoanza tarehe 18-22 Juni 2012.

Changamoto nyingine ni upatikanaji mdogo wa teknolojia bora za uhifadhi na ufungashaji  (grading and packaging) pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu ya umwagiliaji ya kutosha kuongeza uzalishaji wa mpunga alisema Mh. Chiza. 

Aidha,  ukosefu wa  masoko ya uhakika  na teknolojia duni za usindikaji zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi za wakulima kuuza mazao yao yakiwa ghafi badala ya kuuza kama bidhaa.

Katika mkakati huo maeneo ya kipaumbele ni kuboresha uzalishaji wa mbegu bora, umwagiliaji maji, matumizi ya zana za kisasa, uongezaji thamani kwa zao la mpunga, huduma za ugani na utafiti na masuala ya masoko na mikopo katika kuendeleza zao la mpunga.

Ukosefu wa mikopo kwa wakulima, imekuwa inachangiwa kwa kiasi kikubwa na masharti magumu yanayotolewa na taasisi za kifedha, hivyo wakulima kukosa mitaji ya kuwekeza katika  kilimo alisema Mh Chiza. 

Matumizi madogo ya teknolojia rahisi na kasi ndogo ya kusambaa kwa teknolojia miongoni mwa wadau, masuala mtambuka kama maambukizi kwa virus vya Ukimwi na Malaria, pamoja na Ushiriki mdogo wa sekta binafsi katika kilimo ni changamoto  ambazo zinahitaji jitihada maalum katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini,  alihitimisha Mhemiwa Waziri.