Skip to main content
Habari na Matukio

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani Yafana

Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Chakula Duniani yalifikia kilele chake tarehe 16 Oktoba 2015 katika kiwanja cha halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira. 

Maadhimisho hayo yalipambwa na maonyesho na burudani mbalimbali za kwaya na vikundi vya ngoma vikiwa vimebeba ujumbe wa siku ya chakula duniani. Katika maadhimisho hayo, Mheshimiwa Wasira alitembelea na kukagua mabanda ya maonyesho ya bidhaa za kilimo, ufugaji na  uvuvi yaliyokuwa yakionyeshwa na wataalamu na wajasiliamali kutoka taasisi za umma na wadau mbalimbali.

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yalibeba kaulimbiu inayosema “Kilimo na Hifadhi ya Jamii katika Kuondoa Umaskini vijinini.”

Katika hotuba ya kilele cha maadhimisho hayo, Mheshimiwa Wasira alisema kuwa kaulimbiu hiyo inatukumbusha kuwa Serikali inao wajibu wa kutunga Sera na kuandaa program zinazozingatia kutatua matatizo ya kiuchumi, kimazingira na kijamii ili kuondoa uhaba wa chakula na umaskini vijijini.

Akinukuu takwimu zinazotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), mheshimiwa Wasira alisema kuwa, kupitia mipango thabiti ya hifadhi ya jamii, takribani watu milioni 150 duniani kote wamesaidiwa kuondokana na umaskini.

 Alisema kuwa zaidi ya watu milioni 870 duniani kote, mtu mmoja kati ya watu tisa anaishi kwenye njaa ya kiwango cha juu, huku asilimia 60 ya idadi hiyo ya watu wakiwa ni wanawake na zaidi ya watoto milioni 5 duniani kote wako katika hatari ya kufariki kutokana na utapiamlo.

Akizungumzia hali ya chakula nchini Tanzania, Waziri Wasira alisema kuwa, Serikali imeendelea kufanya juhudi kubwa ya kuwasaidia wakulima wadogo, wafugaji na wavuvi ili waweze kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujipatia chakula cha kutosha na lishe bora. Aliendelea kusema  kuwa katika Serikali ya Awamu ya Nne kumekuwa na mikakati na programu mbalimbali ambazo zimetekelezwa na kuchangia kikamilifu katika kukuza kilimo na hifadhi ya jamii.   Alitaja programu na mikakati ambayo ni:- Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDS) wa mwaka 2002; na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) ya mwaka 2006.