Skip to main content
Habari na Matukio

Makampuni ya Pembejeo Fikisheni Pembejeo Haraka kwa Wakulima - Katibu Mkuu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia  Kaduma  ameyahimiza Makampuni yanazoshiriki  kusambaza pembejeo kwa wakulima kwa kutumia  mfumo wa vocha katika msimu wa kilimo wa 2015/2016, kupeleka haraka pembejeo kwa wakulima hususan mbegu bora na mbolea, kwa haraka kwa kuwa msimu wa kilimo umeanza katika maeneo mengi hapa nchini na kuongeza kuwa wanapaswa kufikisha pembejeo hizo hata katika maeneo ambayo msimu wa kilimo haujaanza.

Bibi Kaduma alisema hayo hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Kilimo 1 alipokutana na Wawakilishi wa Makampuni yanazosambaza pembejeo kwa kutumia mfumo wa vocha katika msimu wa kilimo wa 2015/2016.

Aidha Bibi Kaduma alisema, kwa kuzingatia mwongozo uliosambazwa kwa Makampuni hayo na Halmashauri za Wilaya, ya kuwa kila Kampuni, inapaswa kuwasilisha kwenye Halmashauri za Wilaya, orodha ya Mawakala iliyowateua na maeneo, watakayoyafanyia kazi, na  nakala yake iwasilishwe Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika.  

Bibi Kaduma pia, ameyatahadharisha Makampuni hayo kuteua Mawakala waaminifu, na si watakaowahadaa wakulima kwa kuwalipa fedha kidogo ili wasaini vocha bila  kupewa aina yoyote ya pembejeo.

"Mawakala watende haki kwa wakulima, na Kampuni itakayofanya udanganyifu, itawajibika kwa jambo litakalohusiana na usambazaji wa mbegu feki, na mbolea zitakazokuwa chini ya kiwango”. Alisisitiza, Bibi Kaduma.

Bibi Kaduma alihitimisha kwa kuwahakikishia Wawakilishi wa Kampuni za pembejeo kuwa, Serikali itashirikiana nayo katika kufanikisha zoezi zima la usambazaji wa pembejeo kwa kutumia mfumo wa vocha katika msimu wa kilimo wa 2015/2016.