Skip to main content
Habari na Matukio

MGUMBA: WAKULIMA ACHENI KUANIKA MAHINDI CHINI KUEPUKA SUMUKUVU

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewashauri wakulima wa mazao ya mahindi nchini kuacha kuanika mazao yao chini ya ardhi ili kuepuka yasichafuliwe na fangasi wanaosababisha sumukuvu.

Ametoa agizo leo( 14.08.2020) katika kijiji cha Chakware wilaya ya Gairo wakati alipotembelea kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kuzingatia kanuni bora za uhifadhi wa mazao ili kudhibiti tatizo la sumukuvu linaloaathiri mazao hayo.

“ Nipo hapa Gairo kuwahamasisha wakulima wote hususani wale wa zao la mahindi kuacha tabia ya kuanika mahindi kwenye ardhi kwani inapelekea yachafuliwe na fangasi wanaosababisha sumukuvu ambayo ni hatari kwa afya ya wanadamu” alisema Mgumba

Aliongeza kusema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani imejidhatiti kuhakikisha tatizo la sumukuvu kwenye zao la mahindi na karanga linadhibitiwa kwa wakulima na wafanyabiashara kupatiwa elimu.

Naibu Waziri Mgumba amesema Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (Tanzania Initiative To Prevent Aflatoxin Contamination-TANIPAC) unatekelezwa kwenye  mikoa kumi ya Tanzania Bara na miwili ya Zanzibar kwa gharama ya Dola za kimarekani Milioni 35.1  ( sawa na shilingi Bilioni 80) tangu mwaka 2019 .

 “ Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha wananchi wanafundishwa elimu ya kuepukana na sumukuvu ili isiendelee kuathiri maisha ya watu na kupoteza mazao ya wakulima” alisema Naibu Waziri Mgumba

Ametaja faida za mradi huo wa TANIPAC  kwa nchi kuwa utasaidia kuokoa upotevu wa mazao baada ya mavuno kwa kuongeza uhifadhi bora wa mazao na pili utasaidia kuongeza kipato cha mkulima na mfanyabiashara kwa kuzuia sumukuvu kuathiri mazao

Tatu mradi huo umelenga  kuokoa nguvukazi ya watanzania kwa kuhakikisha chakula kinacholiwa kinakuwa hakichafuliwa na fangasi aina ya kuvu .

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe ameiomba wizara ya Kilimo kusaidia kuimarisha ushirika ili wakulima wa zao la mahindi na mazao ya mbogamboga ambayo yanastawi vema wilayani humo kupata soko la uhakika.

Mchembe amesema wilaya ya Gairo ndio inaongozwa kwa uzalishaji wa mahindi kwenye mkoa wa Morogoro ambapo msimu huu 2019/2020 imevuna tani takbribani 40,000 na kuwa uwepo wa mradi wa TANIPAC utaongeza uwezo wa kuhifadhi na wakulima kunufaika.

Akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa ghala la kisasa la kuhifadhi mahindi ,Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) Clepin Josephat amesema ghala litakalojegwa kijijicha Chakware litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 2,000 za nafaka litakapokamilika.

“ Mradi wa TANIPAC utajenga ghala la kuhifadhia nafaka lenye uwezo wa tani 2,000 kwa gharama za shilingi Bilioni Moja  ili kusaidia wakulima kupata mahala pa kuhidadhi mazao yao na kupata elimu ya udhibiti wa sumukuvu katika kipindi cha miaka mitano ya mradi huu” alisema Clepin.

Clepin aliongeza kusema mradi wa TANIPAC umelenga kuhakikisha elimu kwa wakulima juu ya madhara ya sumukuvu inawafikia vijijini na pia kujenga miundombinu bora ya kuhifadhi mazao ili yasichafuliwe na sumukuvu  hivyo kuongeza faida kwa biashara ya mazao.

Mwisho.

 

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

GAIRO

14.08.2020