Skip to main content
Habari na Matukio

Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa Naibu Waziri Ateta na TFRA

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi zao ili kuleta mabadiliko makubwa kwa wakulima.
Akiongea katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Uthibiti wa Mbolea (TFRA) leo na kuwahusisha Watumishi wote wa Taasisi hiyo, Dkt. Mwanjelo amewataka watumishi hao kuwa na malengo na mpango kazi ambao kila mtu atautekeleza  na atapimwa kutokana na mpango kazi huo.
 Hata hivyo Dkt. Mwanjelo amewapongeza  kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa sasa, hususan katika zoezi la uagizaji wa mbolea kwa mfumo wa pamoja (Bulk Procurement System) ambao umechangia kwa kiasi kikubwa mbolea hiyo kumfikia mkulima kwa bei nafuu.
Pamoja na pongezi hizo Naibu Waziri, Dkt. Mwanjelwa ameitaka  TFRA  kuongeza bidii katika utendaji wao wa kazi na kuhakikisha kuwa wanaondoa kero zinazowakabili Wakulima.
Aidha ameitaka Mamlaka ya Uthibiti wa Mbolea kuhakikisha kuwa mambo matatu muhimu yanazingatiwa ambayo ni upatikanaji wa mbolea (Availability) ufikishaji wa mbolea karibu zaidi kwa Wakulima (Accessibility) na kwa bei ambayo wakulima wanaweza kumudu kuinunua (Affordability)
“Mhakikishe mbolea inakuwepo nchini kote na wakulima wanapohitaji inapatikana na iwe kwa gharama ambayo Mkulima anaweza akanunua. “Amekaririwa, Naibu Waziri.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo bwana Lazaro Kitandu amemshukuru Naibu waziri kwa kuwatembelea na kuwatia moyo katika utendaji kazi wao na kumhakikishia kwamba TFRA imejipanga vizuri kupambana na changamoto za baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu hasa katika kuzingatia bei elekezi ya mbolea.