Skip to main content
Habari na Matukio

MHE. MWANJELWA ATEMBELEA WAKALA WA TAIFA WA HIFADHI YA CHAKULA (NFRA) ARUSHA

Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Mary Mwanjelwa hivi karibuni ametembelea Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula – Kanda ya Arusha, zilizopo Mtaa wa Njiro Mkoani Arusha ili kujionea namna wanavyofanya kazi kutekeleza majukumu yao.

Mhe. Mwanjelwa ametembelea Ofisi hizo ambapo pamoja na mambo mengine amekagua maghala yanayotumika kuhifadhi chakula ambapo amejionea ukubwa wa maghala hayo na jinsi kanda ya Arusha ilivyo na uwezo wa kuhifadhi chakula wastani wa Tani 39,000.

Pia alijionea akiba kubwa ya mahindi iliyopo ghalani  katika msimu huu wa mwaka 2017/2018 ambayo ni Jumla ya tani 3,997.664 ambazo hizo ni pamoja na salio la mahindi la msimu uliopita wa  2016/2017 ambazo zilikuwa Tani 2,997.664

Akizungumza na Watumishi wa NFRA – Kanda ya Arusha, Mhe. Mwanjelwa aliwapongeza kwa uwajibikaji huku akiwasihi kuongeza ufanisi na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuzikabili changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya ufinyu wa bajeti.

Mhe. Mwanjelwa amesema kuwa sifa ya Mtumishi mzuri ni yule mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto ili kutimiza adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika kukuza ufanisi katika kazi kwa kutimiza vyema wajibu kwa kuwa wabunifu.

Amesema kuwa Watumishi wanapaswa kuongeza ushirikiano na Ari mpya ya kazi kwa kufanya kazi kwa weledi kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

Chimbuko la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula lilitokana na lililokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) mwaka 1990 ambapo dhumuni kubwa ilikuwa ni kuwepo na Kitengo maalumu cha kununua, kuhifadhi, kuhudumia chakula sehemu zenye upungufu wa chakula na kulinda bei ya soko la mahindi kwa mlaji mbali na shughuli zilizokuwa zikifanywa na NMC.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula ipo chini ya Wizara ya Kilimo na Msimamizi Mkuu wa shughuli zote za Wakala ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala (CEO).