Skip to main content
Habari na Matukio

Minada Sita ya Korosho Yaingiza Zaidi ya Shilingi Bilioni 406.3

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

 

Zao la korosho katika msimu wa kilimo mwaka 2019/2020 limeingiza zaidi Shilingi Bilioni 406.3 kupitia minada sita ambayo imekwishafanyika kwa nyakati tofauti nchini.

 

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo (Ijumaa 13 Disemba 2019) mjini Mtwara wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa ofisini kwake mara baada ya kuwasili mkoani Mtwara kwa lengo la kufuatilia malipo ya wakulima wa korosho.

 

Waziri Hasunga amesema yupo mkoani Mtwara kufuatilia hali ya malipo ya korosho kwa wakulima na watoa huduma tangu msimu wa ununuzi wa zao hili ulipoanza mwezi Novemba mwaka huu kupitia mfumo wa wazi wa zabuni za wazi ulipoanza.

 

 “Tayari tani 163,000 za korosho zimekusanywa huku tani 151,554 zikiwa zimeuzwa katika minada sita iliyofanyika nchini.”Alisema Waziri wa Kilimo

 

Hasunga amesema hali ya minada inayoendelea inatoa taswira chanya kwa wakulima, hivyo kuwa na uhakika wa kipato cha korosho zao kutokana na bei kupanda kwani korosho ni zao muhimu na ndilo linaongoza kwa kuiingizia nchi pato kubwa la kigeni likifuatiwa na zao la Tumbaku.

 

“Bado tunaendelea na minada lakini hadi sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 406 zimepatikana kwa wakulima hali inavyoonyesha maendeleo mazuri” alikaririwa Waziri Hasunga

 

Waziri huyo amesema serikali inachukua hatua za dhati kuhakikisha Ushirika unasimamiwa ipasavyo ambapo Ushirika unaonekana kuimarika zaidi kwenye mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kuliko maeneo ya yanayolima zao la Pamba na Kahawa.

 

Kuhusu ubadhirifu kwenye vyama vya ushirika nchini, Waziri Hasunga amesema tayari wizara ya kilimo imeanza kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika ambao wamepokonya mali za wana ushirika.

 

Waziri wa Kilimo yupo mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi akitokea mkoani Lindi ambapo pamoja na mambo mengine atakagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020 na kukagua skimu za umwagiliaji.

 

MWISHO