Skip to main content
Habari na Matukio

Mkakati wa Kuendeleza zao la Muhogo Tanga Waanza

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo Idara ya Uendelezaji  Mazao  pamoja na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini  leo wamedhuru Mkoa wa Tanga lengo likiwa ni kuangalia namna ya uendelezaji wa  zao la muhogo mkoani humo na changamoto zinazolikabili.

Akiongea na timu hiyo  Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi Zena Ahamedi  Saidi amesema,  mkoa wa Tanga umekuwa na mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza zao hilo ambapo kila nyumba ilitakiwa kuwa na ekari moja ya muogo ili kuimarisha usalama wa chakula mkoani humo.

Aidha mipango imeendelea kufanyika baina ya mkoa  na Taasisi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili waweze kuzalisha mbegu ya kutosha  na kuzisambaza kwa wakulima,alisisitiza Bi Zena.

Hata hivyo aliendelea kusema kwamba bado upatikanaji wa soko ni changamoto kubwa kwa wakulima kwani bado hawajapata soko la uhakika.

Naye mkuu wa msafara na mtaalamu wa mazao ya bustani bi Tabu Likoko amewaeleza kwamba  kupitia mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) zao la muhogo limepewa kipaumbele kwakuwa ni moja ya mazao ya biashara na  chakula hasa katika mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara  na sehemu nyinginezo.

Akijibu changamoto ya soko Bi Tabu amesisitiza kwamba  tayari nchi ya china na Tanzania wameingia kwenye itifaki ya uzalishaji wa zao la muhogo na kuliuza nchini china hivyo serikali inaangalia namna nzuri ya kuzishirikisha sekta binfsi  ili zishiriki kikamilifu katika kuingia mikataba na wakulima wanaozalisha muhogo.

Naye mkulima wa mbegu za muhogo  kutoka kijiji cha Parungu kata ya Kasela Wilaya ya Mkinga  Bwana Ilale Protasi   ambaye ana shamba lenye ukubwa wa ekari saba (7) zilizopandwa muhogo anasema  amepata faida kubwa kutokana na kilimo cha mbegu za muhogo  ambapo kimemuwezesha kubadili maisha na kuwasomesha watoto wake.

Aidha bwana Ilale ameiomba serikali kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupata soko la uhakika na uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo vya kuongeza thamani ya zao hilo ili kuepuka hasara ambazo  zimekuwa zikipatikana kwa kuuza mihogo kwa bei ya chini.