Skip to main content
Habari na Matukio

MRADI WA UMEME WA NYERERE NI FURSA YA KILIMO KWA VIJANA-MGUMBA

Serikali imesema kukamilika kwa mradi wa kufua umeme wa Nyerere katika mto Rufiji ni fursa ya uhakika ya vijana kufanya kazi ya kilimo cha umwagiliaji kwa tija zaidi.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amesema hayo leo (27.02.2020) Mkoani Njombe wakati alipofungua kongamano la vijana kujadili fursa za  kilimo kwa mikoa ya Njombe,Iringa na Ruvuma

“Mradi wa umeme wa Nyerere (Rufiji Hydro) utakapokamilika utasaidia kudhibiti mafuriko,hivyo itakuwa fursa kwa vijana kuzalisha mazao ya kilimo kwa wingi kwa kutumia umwagiliaji” alisema Mgumba

Aliwasihi vijana kujipanga na kutumia elimu toka kwa wataalam wa kilimo na maafisa ugani ili eneo la ekari 150,000 katika bonde la mto Rufiji zitumike kuzalisha ajira katika kilimo na uvuvi

Naibu Waziri huyo amesema vijana toka mikoa yote nchini wajiandae kutumia eneo hilo la mto Rufiji kukuza sekta ya kilimo na mifugo kwani Serikali ya awamu ya Tano itakamilisha mradi huo mwaka 2021.

 “Katika kipindi cha miaka minne tu ya uongozi wa Rais Dkt.John Pombe Magufuli imeweza kufanikiwa kuongeza eneo la ekari 150,000 za kilimo cha umwagiliaji kupitia mradi wa Umeme wa Nyerere katika mto Rufiji” alipongeza Mgumba

“Vijana twendeni Rufiji siyo mbali,fursa za kilimo zipo za kutosha” alisema Naibu Waziri Mgumba

Tanzania kwa miaka mingi sasa imetumia eneo la hekta 475,000 pekee kati ya hekta milioni 29,4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini.

Mgumba ametaja fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo kuwa ni eneo la kutosha na ardhi nzuri ,pili uwepo wa mahitaji makubwa ya mbegu bora hivyo wanaweza kuanzisha mashamba ya mbegu

Tatu,serikali imefikisha umeme kwenye vijiji 9000 kati ya 12,268  hivyo ni fursa ya kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo kwani soko lipo

Alitaja fursa ya  kuzalisha mazao ya alizeti,karanga,pamba,ufuta na nazi kuzalisha mafuta ya kula

“Nchi inahitaji mafuta ya kula lita 650,000 kwa mwaka lakini uzalishaji wetu ni lita 250,000 huku viwanda vilivyopo vina uwezo wa kuchakata lita milioni mbili ,hii fursa tachangamke” alisema Mgumba

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mgumba alisema Kilimo kimeendelea kukua na kutoa mchango kwa uchumi wa nchi katika maeneo mbalimbali.

Takwimu zinaonesha kuwa sekta ya kilimo imechangia asilimia 28.2 ya pato la Taifa ambapo Sekta ndogo ya Kilimo inayojumuisha mazao ya biashara, mazao ya bustani na mazao mengine (nafaka, mikunde na mazao ya mafuta) ilichangia kwa asilimia 16.2 ya pato la Taifa kwa mwaka 2018.

Aidha, katika kipindi hicho Sekta ya Kilimo imetoa ajira kwa watanzania asilimia 58, imechangia asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje na inachangia kwa asilimia 100 ya mahitaji ya chakula nchini.

Akiwasilisha mada, Mratibu wa Mradi wa Vijana katika kilimo( EAYIP) toka ESRF Patrick Kihenzile amesema wamefanikiwa kuweka mazingira wezeshi ili kuongeza ushiriki wa vijana kwenye sekta ya kilimo biashara na mnyororo mzima wa thamani.

Kihenzile alitaja changamoto za vijana kushiriki kilimo kuwa  uelewa mdogo wa mahitaji ya Kisera, Sheria na Mikakati ili kuwa na mazingira mazuri ya kilimo biashara.

Changamoto nyingine ni uelewa mdogo jinsi ya kupata mikopo kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wa halmashauri na tatu ni vijana waliowahi kukopa walisema pesa zinazotolewa zilikuwa kidogo mno kukidhi mahitaji.

“Vijana wengi wamekuwa wakisema wanapewa mitaji kidogo isiyokidhi gharama za uzalishaji mashambani” alieleza Kihenzile

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri aliijibu hoja za vijana kuchelewa kupatiwa mikopo alisema ni wakati sasa Halmashauri zote za mkoa wa Njombe zikaacha urasimu wa kuchelewesha mikopo

“Halmashauri punguzeni urasimu ,msikae zaidi ya robo mwaka bila kutoa mikopo ili vijana wanufaike na fedha za serikali” alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe.

Msafiri aliongeza kusema ili vijana wafanikiwe kawenye kilimo ni budi viongozi na watendaji wa serikali wakawa na imani na vijana kuwa wanaweza kuzalisha ajira kupitia kilimo na kuonya tabia za baadhi wa watendaji kuwadharau vijana

Msafiri alisema Rais wa Awamu ya Tano Dkt.John Pombe Magufuli ana imani kubwa sana na vijana ndio maana ameteua wengi kushika nafasi za uongozi na kwamba ni fursa za vijana kutumia taaluma na uwezo wao kukuza uchumi.

“Sisi nasi tulikuwa vijana,tulilelewa na tuliaminiwa ndio maana leo tumepewa uongozi na Rais Magufuli” alisema Msafiri.

Naye kijana Tulizo Ngata kutoka kata ya Mdandu halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe akitoa salamu kwa niaba ya wenzake aliipongeza serikali kwa kupitisha sheria ya halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya vijana(4%),wanawake (4%) na walemavu (2%) kuwa imesaidia kukuza kazi za kilimo na mifugo vijijini.

Kijana huyo aliongeza kuwaomba viongozi hususan mawaziri kwenda vijijini kutembelea miradi ya vijana ili wasaidie kutatua changamoto za upatikanaji pembejeo,mbolea,madawa na masoko kwa mazao

“Tunaomba Naibu awaziri Mgumba usiishie hapa Njombe ufike hadi Wangin’ombe tunakofanya kazi za kilimo na mifugo uone kazi zetu na utusaidie zikue zaidi” alisema Tulizo,

Akizungumza awali Mratibu wa Vijana toka Wizara ya Kilimo na Mratibu wa Kongamano haya  Revelian Ngaiza alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza Mkakati wa Miaka Mitano wa Taifa kwa Vijana kushiriki katika sekta ya kilimo (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture- NSYIA) wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Ngaiza alisema utekelezaji wa Mkakati huo unashirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Ametaja wadau wengeine kuwa ni Jukwaa Huru la wadau wasio wa Serikali(ANSAF),Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II),ESRF,SUGECO,PASS,RUDI,AGRIPROFOCUS,HEIFER International,RUDI,IECA,NMB na CRDB

Jumla ya makongamano saba yatafayika katika kanda saba za Songwe,Njombe,Tabora,Arusha,Mara na Geita ambapo uzinduzi rasmi ulifanyika tarehe 24 Februari 2020 Songwe na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ambapo vijana 680 walishiriki.

Makala hii imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

NJOMBE

27.02.2020