Skip to main content
Habari na Matukio

Msukumo wa Pamoja ni Muhimu Katika Kuongeza Uzalishaji wa Mpunga

Wakulima wametakiwa kuweka msukumo wa pamoja ili kuhakikisha kwamba zao la mpunga linaendelezwa kwa kiwango kikubwa ili kuinua kiasi cha uzalishaji na kuongeza usalama wa chakula na kipato. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mh. E.ng. Christopher Kajoro Chiza alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakulima waliohudhuria maadhimisho ya maaonyesho ya zao la mpunga yaliyofanyika katika uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es salaama.

Aidha msukumo huo utawasaidia wakulima kuendeleza uchumi na kuwakwamua wananchi walioko katika ukanda wa mashariki mwa Afrika kutoka kwenye umaskini hususan kwa wakulima wadogo ambao wanahitaji kupata teknolojia mbalimbali zinazoweza kuwasaidia katika kuongeza uzalishaji na tija.

‘Hapa kwetu tunatambua umuhimu wa zao la mpunga. Zao hili ni la pili kwa uzalishaji katika mazao ya nafaka baada ya zao la mahindi na hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Mwanza, Mbeya, Rukwa, Morogoro, Arusha, Manyara, Iringa, Mara, Tanga na Kigoma. Aidha uzalishaji wa mpunga unaongezeka mwaka hadi mwaka na takwimu zinaonyesha kwamba eneo la uzalishaji liliongezeka kutoka hekta 490,000 mwaka 1998 mpaka hekta 854,000 mwaka 2011’. 

Waziri alisema kuwa  mwaka 2010/2011 uzalishaji wa Mpunga ulifikia wastani wa tani 2,213,020.  Hii inaonyesha uzalishaji wa mpunga unaongezeka kwa kasi kubwa kutokana na kuongezeka kwa ruzuku kwenye mbegu, mbolea pamoja na kupanuliwa kwa eneo la umwagiliaji ambalo kwa sasa limefikia hekta 381,000 ambalo kwa sehemu kubwa linalimwa zao la mpunga. 

Inakadiriwa kuwa ongezeko la matumizi ya zao la mpunga kama chakula duniani ni zaidi ya asilimia 6 kwa mwaka. Kwa Tanzania mahitaji yetu ya mchele kwa mwaka 2009/2010 yalikuwa tani 788,570 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 1,699,830. Mwaka 2010/2011 mahitaji yaliongezeka na kufikia  tani 816,648 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani 1,461,648 alisema Mh. Chiza.