Naibu Katibu Mkuu Afungua Mkutano wa Kanda wa Mradi wa EAAPP EAAPP
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Eng. Raphael Daluti hivi karibuni alifungua mkutano wa 10 wa Mashariki mwa Afrika wa kuhitimisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa EAAPP.
Katika hotuba yake, Eng. Daluti alisema, kuna mambo mengi ya kujivunia kutokana na matokeo ya utekelezaji wa mradi katika kipindi cha miaka mitano huku akitaja maeneo ambayo yamekuwa na ongezeko la uzalishaji wa maziwa, mazao ya mpunga, mihogo na ngano.
Eng. Daluti aliongeza kuwa eneo lililoonyesha mafanikio wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ni ongezeko la wataalam katika eneo la utafiti. Mradi umefanikisha ufadhiri katika tafiti kadhaa na kuongeza kuwa zaidi ya Watafiti 110 kwenye ngazi mbalimbali walishiriki huku zaidi ya Watafiti 6 kwenya ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD) na Watafiti 16 kwenye shahada ya Uzamili (Masters Degree) walifadhiriwa na kusoma kwenye vyuo mbalimbali.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mshikamano wa Kikanda katika maendeleo ya sekta ya kilimo kwani kumekuwa na juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto zinazomkabili mkulima wa Afrika. Alipongeza juhudi hizi kuwa ni namna nzuri ya kujiandaa kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu, ambapo, inafikiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 dunia itakuwa na watu zaidi ya bilioni 9.1 ambao watahitaji chakula ambacho kwa sehemu kubwa, kinazalishwa Afrika.
“Wote, tunafahamu namna ambavyo malengo ya mradi wa EAAPP yalivyotekelezwa kwa vitendo na matokeo, yameonekana kwenye, kuongeza tija na uzalishaji lakini pia kuongezeka kwa ushirikiano katika kuboresha teknolojia na mafunzo ya wataalam. Hayo yamechangiwa na jinsi ambavyo nchi zetu, zilivyoshirikiana katika upeanaji wa taarifa za kimkakati katika mazao manne ya kipaumbele ambayo, ni mpunga, ngano, mihongo na uzalishaji wa maziwa.” Alisema Eng. Daluti.
Mradi wa EAAPP ulikuwa ukitekelezwa na taasisi za kilimo na mifugo katika nchi nne ambazo ni Ethiopia, Kenya, Tanzania na Uganda kwa mazao ya ngano, maziwa, mpunga na muhogo.
Mradi huo ulikuwa na malengo ya kuzalisha teknolojia kupitia utafiti wa mazao ambayo ni ngano, mpunga, muhogo na maziwa, pia kuzisambaza kwa walengwa ambao ni wakulima na wafugaji.
Tangu mradi wa EAAPP ulipoanzishwa miaka minne iliyopita zaidi ya teknolojia 400 zimepatikana na kusambazwa kwa wakulima na wafugaji.
Akizungumza katika mkutano huo, mtalaam kutoka Kenya Dkt. David Wekesa Nyongesa alisema mradi huo umewawezesha kuzalisha mbegu za mifugo ambazo zimeanza kuwa na mahitaji makubwa ndani na nje ya Kenya.
Mradi wa EAAPP ulianza kutekelezwa mwaka 2010 na utafikia tamati ya awamu ya kwanza, tarehe 31, Desemba, mwaka huu.