Skip to main content
Habari na Matukio

Naibu Waziri atembelea Mkoa wa Kigoma

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Eng. Christopher Chiza  hivi karibuni alimaliza ziara ya kikazi ya  siku sita katika  Mkoa wa Kigoma katika Wilaya za Kigoma Vijijini, Kibondo,na Wilaya mpya ya Kakonko.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri alifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa usambazaji pembejeo  ya ruzuku ikiwa ni pamoja  na kupata maelezo na changamoto zilizojitokeza katika utaratibu mzima wa usambazaji wa pembejeo hizo. Moja ya changamoto kubwa iliyoelezwa na baadhi ya wakulima, ni kwa wakulima  kuweka sahihi kwenye vocha bila ya kuchukua  pembejeo husika kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipia  pembejeo zikiwemo mbegu bora na mbolea

Aidha Mhe. Eng. Chiza aliuagiza  uongozi wa wilaya husika  kufanya ufuatiliaji wa karibu katika zoezi  zima la usambazaji wa pembejeo ili kubaini baadhi ya mawakala ambao sio waaminifu. Katika ufuatiliaji huo kila mkulima aliyeweka saini kwenye vocha itabidi athibitishe kuwa alipokea  pembejeo, na kasha kuonyesha shamba lake zilipotumika  pembejeo hizo.

Mhe Eng. Chiza  vile vile alipata fursa  ya kutembelea wakulima wa zao la kahawa katika kijiji cha Muhange , Shughuli za kilimo cha umwagiliaji na katika kijiji cha Nyamtukuza na Kituo  cha mpakani cha Mabamba katika wilaya ya Kibondo kinachoshughulikia  Ukaguzi wa Mazao na Afya ya Mimea.