Skip to main content
Habari na Matukio

NAIBU WAZIRI BASHE AONGOZA ZOEZI LA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA KUONGEZA TIJA NA UZALISHAJI WA PAMBA

NAIBU WAZIRI BASHE AONGOZA ZOEZI LA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA KUONGEZA TIJA NA UZALISHAJI WA PAMBA MWAKA 2021

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (Jana) tarehe 17 Januari, 2021 ameongoza tukio la kihistoria la utiaji saini mkataba wa kuongeza tija na uzalishaji (Performance Agreement) wa zao la pamba mwaka 2021 kati ya Bodi ya Pamba, Vyama vya Ushirika na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Awali Waziri Bashe amesema tija ya sasa kwa Wakulima wengi wa zao la pamba katika mikoa mingi ni kilo 200 wakati tija inapaswa kufikia angalau kilo 800 kwa heka.

Mkataba huo umejikita katika makubaliano ya matumizi ya pembejeo za pamba za msimu wa pamba wa 2020/2021.

“Zao la pamba ni kila kitu kwa Wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa; zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati katika Awamu ya Tano. Uzalishaji wenye tija katika zao la pamba unahitaji upatikanaji wa pembejeo mbalimbali ikiwemo mbegu, mbolea na viuadudu”. Amekaririwa Naibu Waziri Bashe.

Lengo la mkataba huo ni kuhakikisha pembejeo zinapatikana na zinasambazwa kwa Wakulima kwa wakati kupitia mfumo wa ushirika na zinatumika ipasavyo ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la pamba kwa msimu wa 2021.

Naibu Waziri Bashe amesema Serikali imeazimia kuongeza uzalishaji wa zao la pamba kwa kuhamasisha matumizi sahihi ya pembejeo na hivyo kutoa maelekezo kwa Bodi ya Pamba, Vyama Vikuu na Vyama vya Msingi (AMCOS) kuingia makubalaiano ya matumizi sahihi ya pembejo za pamba kwa msimu wa 2021.

“Wakulima wa zao la pamba watasambaziwa pembejeo kwa kuzingatia uzalishaji na mahitaji ya pembejo husika kupitia Vyama vyao vya Msingi (AMCOS)”.

Naibu Waziri Bashe amesema Wakulima watasambaziwa pembejeo kupitia AMCOS zao kwa kuzingatia makadirio ya uzalishaji na idadi ya Wakulima kwa mchanganuo wa aina ya mbolea (Mbegu/Mbolea na Viuadudu kwa kiasi cha idadi ya mbegu, mbolea na ujazo wa viuadudu husika. Kati ya Bodi ya Pamba na Vyama Vikuu na Vyama Vikuu na Vyama vya Ushirika vya Mazao (AMCOS).

Aidha; Naibu Waziri Bashe amesema kupitia tani elfu 12 (12,588) za mbegu bora zilizosambazwa kwa Wakulima nchi nzima; Matarajio ya kitaifa ni kuzalisha pamba tani laki 5 kwa nchi nzima kwa msimu wa kilimo wa 2021.

“Uzalishaji wetu kwa mwaka huu usipungue tani laki 5(500,000) nchi nzima. Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anafanya kwa sehumu yake na inawezekana kabisa kuzalisha hadi tani milioni 1”. Amemalizia Naibu Waziri Bashe.