Skip to main content
Habari na Matukio

“NFRA TOENI HUDUMA, FANYENI BIASHARA, NA JIENDESHENI KWA FAIDA” – KATIBU MKUU KILIMO

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bwana Gerald Musabila Kusaya amewataka Watumishi wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa kufanya kazi kwa ubunifu ili kuifanya Taasisi hiyo ijiendeshe kwa tija na ufanisi mkubwa.

Katibu Mkuu, ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembela Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha, kujifunza namna Watumishi wa Taasisi hizo wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Watumishi wa NFRA Kanda ya Kipawa, Bwana Gerald Kusaya, kwanza amewapongeza Watumishi wote kwa namna wanavyojitoa katika kutekeleza majukumu yao lakini pia amewataka kuwapa ushirikiano Viongozi wao na kuendelea kufanya kazi kama timu na familia moja.

“Fanyeni kazi kama timu, hiyo ndiyo siri ya mafanikio lakini pia napenda mfahamu kuwa Mimi kama Kiongozi wenu; nipo na ninawaunga mkono”. Amekaririwa Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Taasisi ya NFRA Kanda ya Kipawa ina jukumu kubwa la kuhifadhi chakula kwa ajili ya kuhudumia mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara na kuongeza kuwa licha ya kutoa huduma kwa Watanzania lakini kuna haja ya kuongeza ubunifu kwa kujiendesha kibiashara.

“Nafahamu, mnatoa huduma kwa Watanzania, lakini Mimi kama Katibu Mkuu wenu; nawashauri mtoe huduma lakini pia fanyeni biashara na mwisho wa siku msipate hasara”.

“NFRA ni Taasisi inayofahamika, nendeni Benki ili mkope fedha kwa ajili ajili ya kuendesha miradi mikubwa ya biashara na siku hizi tuna benki maalum inayohudumia Sekta ya Kilimo Mazao, Benki ya Kilimo (TADB) itumieni, na binafsi nipo kama mtapata changamoto yoyote; njooni hata bila mihadi (Appointment) na nitawaunga mkono.” Amekaririwa Katibu Mkuu.

Wakati huohuo Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amewahakikishi Watanzania kuwa Taifa lina akiba ya kutosha ya chakula na kwamba licha ya changamoto ya ugonjwa wa homa ya mapafu, unaosababishwa na kirusi ina ya “Corona” akiba ya chakula ya taifa, ina chakula cha kutosha.

“Niwahakikishe Watanzania wenzangu kuwa Taifa letu linachakula cha kutosha na kuna maeneo yanauzalishaji mzuri kwa kuwa yalipata mvua za vuli na yanaendelea kupata mvua za masika vizuri”. Amemalizia Katibu Mkuu.