Skip to main content
Habari na Matukio

NFRA YAKABIDHI GAWIO LA MILIONI 500 KWA SERIKALI

Na. Issa Sabuni-WK, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameipongeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa kutoa gawio la Shilingi Milioni 500 kwa serikali kitendo kinachoonyesha kuwa taasisi hiyo inajiendesha kwa faida na tija.

Dkt. Mpango aliyasema hayo wakati wa hotuba yake, baada ya kupokea gawio na michango ya fedha zilizotolewa kwa Serikali kutoka kwa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi 13 kwenye hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Kilimanjaro katika Jengo la Wizara ya Fedha, Jijini Dodoma jana (08.01.2020).

“Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru kwa kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, nataka niwahakikishe kuwa fedha hizi, zitarudi kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia Watanzania wanyonge”. Amekarirwa Waziri Mpango.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imetoa mchango wake wa shilingi milioni 500 kwa Serikali mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ambaye aliambatana na Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Msajili wa Hazina Athumani Mbuttuka.

Akiongea wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano ya hundi za mfano, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alisema inatia moyo kuona Wenyeviti wa Bodi pamoja na Wakuu wa Taasisi, Wakala na Mifuko na Vyuo vya Elimu ya Juu ambao wametoa gawio na michango yao kwa Serikali, yenye jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.

 “Wito wangu na matarajio yangu ni kuwa mwaka ujao, mtajiangalia zaidi ili tupate zaidi kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi wetu”.

Waziri Mpango ameongeza kuwa kwa sasa duniani nchi zilizokuwa zikitoa misaada kupitia Mfuko Mkuu wa Dunia (Global Fund) hazifanyi hivyo, zaidi zimejikita katika kutoa misaada hiyo kwa nchi zao zaidi na kwamba ndiyo maana ni lazima nchi zinazoendelea kama Tanzania zijifunge mkanda kwa kutumia rasilimali zao.

Akiongea baada ya hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Milton Lupa alisema, amefurahishwa kuona NFRA imetii agizo la Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutoa mchango wa shilingi milioni 500 ambapo fedha hizo, zinaenda kwenye miradi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Napenda kuwapongeza Watumishi wote wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa pamoja, tumefanikisha jambo hili, furaha yangu ni kuwa michango hii, inaenda kwenye miradi ya kimkakati, ambapo Taifa zima tutanufaika kwa rasilimali zetu”. Amekaririwa Bwana Lupa.

Katika hatua nyingine Dkt.Mpango amewakumbusha na kuwaonya, Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa zile Taasisi Thelasini na Sita (36) ambazo hazijatoa gawio na michango yao hadi sasa kuwa ifikiapo tarehe 23 Januari, 2020 saa 6 usiku, wasingoje barua za kuachishwa kazi toka kwake bali tarehe 24 Januari, 2020 wasiwepo Ofisini kwa kushindwa kutekeleza agizo la Rais Magufuli.

“Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 55 hatutakosa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi kuchukua nafasi zao, katika jambo hili, hakuna utani” Alimalizia Waziri Mpango.

Mwisho.