“Nitawalinda watendaji wangu wakitekeleza majukumu yao” Waziri Bashe
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema kuwa ataendelea kuwalinda na kuwatetea wafanyakazi wa wizara ya kilimo wakiwemo wanaohudumu kwenye Taasisi na Bodi za wizara katika utekelezaji wa majukumu yao kulenga kuleta tija kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Waziri Bashe ametoa rai hiyo wakati akizungumza na Wenyeviti na Watendaji wa Bodi pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo kwenye kikao kilichofanyika leo Oktoba 31 Jijini Dodoma.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimelenga kutoa mwelekeo wa Sekta ya Kilimo katika kuendeleza utekelezaji wa malengo yaliyopangwa katika mwaka huu wa fedha 2023/2024.
Waziri Bashe amesema kuwa anatambua mchango wa kila mtendaji katika kuendeleza sekta ya kilimo na kuwa kuna wakati kunakuwa na changamoto kadhaa zinazokwamisha utendaji kazi wao zikiwemo changamoto za kisiasa na katika mazingira hayo Waziri Bashe ameahidi kukaa upande wa wafanyakazi.
Pia Mhe. Waziri Bashe katika kutoa mwongozo wa kazi, amewahamasisha watendaji kubuni mbinu mbalimbali za utendaji ili kufikia matarajio ya Serikali ya kuhudumia wakulima na kuinua hali ya uzalishaji wa mbegu bora na chakula nchini.
Waziri Bashe, amewataka watendaji hao kusimamia majukumu kikamilifu huku wakitambua kuwa wanalo jukumu la kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo kwa kuwawezesha kulima kisasa.
"Nataka niwaambie Wenyeviti wa Bodi, mkikaa na baadhi ya wataalamu wa kilimo, baadhi ya malalamiko mtakayopokea ni pamoja na wakulima hawataki kulima kisasa. Lakini suala la kujiuliza, ni je tunatatua changamoto zao zinazowakwamisha kulima kisasa, na tunawawezeshaje kupata mbegu bora, yani ni jukumu lenu kuhakikisha wakulima wanalima kisasa” amesema Mhe. Waziri Bashe.
Pia Waziri Bashe amewataka Watendaji wakuu wa Taasisi kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi kwenye Taasisi na Bodi husika anajua sera na malengo ya wizara katika kutoa huduma hatua itakayopelekea wafanyakazi kutambua thamani na majukumu yao.
Aidha, Mhe. Waziri amewataka watendaji kujenga tamaduni za kufanya kazi kwa pamoja na kufahamiana maeneo waliyopewa ili kazi za kutoa huduma kwa wakulima ziwe na ufanisi zaidi.
"Kuanzia bajeti ya mwaka 2024/2025 tutajenga majengo ya Ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kila Mkoa; na ndani yake zitakuwepo ofisi nyingine za kilimo kama vile ofisi ya taasisi za mbegu, afya ya mimea, na nyingine ili zifanye kazi kwa pamoja na kumhudumia mkulima kwa ukaribu,” ameongeza Mhe. Waziri Bashe.