Skip to main content
Habari na Matukio

RAIS MAGUFULI AMENITUMA NIWALETEE ZAWADI YA MIRADI MIWILI – KATIBU MKUU GERALD KUSAYA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya amewaambia Wananchi wa kijiji cha Mtanana B kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kuwa ametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwaletea zawadi ya ujenzi wa Kituo Mahiri (Centre of Excellence) kwa ajili Udhibiti wa Sumukuvu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo ambalo Kituo Mahili (Centre of Excellence) cha Ujenzi wa Mradi huo kinataraji kujengwa na kuongeza kuwa tayari fedha kwa ajili ya ujenzi huo ilishatolewa na Mhe. Rais na kwamba kinachosubiriwa ni Wananchi kuridhia na kutoa eneo la ekari 150 na baada ya hapo kesho tarehe 18 Juni, 2020. Serikali itasaini makubaliano na Kampuni ya ujenzi ya B.J. Amuli ambayo itajenga majengo ya mradi huo.

Ujenzi wa Mradi wa Kituo Mahili cha Udhibiti wa Sumukuvu unaenda sambamba na ujenzi wa Maabara Maalum itakayotumika kupima sampuli na kuendesha majaribio mbalimbali yenye lengo la kuongeza mapambano ya udhibiti wa changamoto ya sumukuvu.

Baada ya maelezo hayo ya Katibu Mkuu; Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtanana B Bwana Zakaria James amesema Wanakijiji wamekubali mradi huo kujengwa katika eneo lao na kwamba watajitolea kuhakikisha mradi unalindwa na unafanikiwa kama ilivyopangwa.

“Katibu Mkuu; naomba tufikishie salama zetu kwa Mhe. Rais Magufuli. Tumekubali mradi huu uanze na tunaahidi kuulinda ili ufanikiwe sawa sawa na malengo yake.” Amekaririwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mtanana B.

Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mtanana B amesema Wananchi wameunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo na kwa kauli moja wamekubali kutoa eneo la ekari 150 ili kuhakikisha ujenzi unaanza na kukamilika kwa wakati.

Akiongea mbele ya Katibu Mkuu; Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Bwana Omary Nkullo amesema kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Kongwa, anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli na kuongeza kuwa Kongwa imekuwa ikipata fursa ya kutekeleza miradi mingi na kwamba Viongozi watahakikisha wanashirikiana na Mkandalasi ili ikamilike kwa wakati.

Awali Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya alitembelea ili kuona eneo itakapojengwa mradi wa pili wa ujenzi wa maabara maalum katika eneo la Mahoma Makulu njia ya kuelekea Hombolo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Baada ya kufika na kukagua eneo la ujenzi wa maabala hiyo maalum kwa ajili ya kufanyia majaribio ya sampuli za sumukuvu Bwana Kusaya amesema eneo lipo sehemu nzuri na kuongeza kuwa ni vyema Mjenzi atakayejenga maabara hiyo pamoja na majengo mengine kuhakikisha kuwa anajenga majengo yenye viwango na kulitumia eneo vizuri huku msisitizo ni kufanya usafi wa eneo husika kwa kutokata miti yote ya asili ili kulinda uasili na kutunza mazingira.

“Mkandalasi (Kampuni ya K & M Architect) napenda kusisitiza kuwa matumizi mazuri ya nafasi wakati wa ujenzi ili kama Wizara itakuwa na mahitaji mengine basi eneo litumike kwa ufanisi” Amekaririwa Katibu Mkuu.

“Jambo lingine, ni vyema eneo hili lisafishwe vizuri bila kuleta uhalibifu wa mazingira, kuna miti ya asili ambayo si vyema ikikatwa yote; Sisi Wizara ya Kilimo ni Wadau wa mazingira, lazima tuonyeshe kwa vitendo dhana ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira”. Amesisitiza Bwana Kusaya.

Katibu Mkuu baada ya kufanya ukaguzi wa eneo la ujenzi wa maabara hiyo ametoa maagizo ya kuanza mara moja kwa usafishaji wa eneo husika kwa kuzingatia maelekezo hayo na kuahidi kuwa usafi utakapokamilika, atakuja kutembelea ili kujionea maendeleo ya kazi hiyo.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilizindua rasmi Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANPAC) mapema mwezi Julai 2019 ambapo, utekelezaji wa Mradi huo ni pamoja na ujenzi wa Kituo Mahili cha Udhibiti na mafunzo ya sumukuvu pamoja na maabara kwa ajili ya kupimia sampuli pamoja na kuendesha utafiti huku msisitizo ukiwa ni mikoa inayoathirika mara kwa mara. Mikoa hiyo ni pamoja na Dodoma na Manyara