Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI KUJENGA SKIMU ZA UMWAGILIAJI NA MABWAWA MBARALI.

Wizara ya Kilimo chini ya Serikali ya awamu ya 6 ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa inafikia malengo ya kukuza Sekta ya Kilimo kwa asilima 10 ifikapo mwaka 2030, baada ya Maboresho ya Mpaka GN 28 sambamba na tamko la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa la kuchora Mpaka mpya, inakwenda kujenga mabwawa makubwa 6 na Skimu za umwagiliaji za kisasa 8 kwenye eneo la ekari 91,231 lililotengwa kwa ajili ya kilimo Wilayabi Mbarali,Mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde wakati wa Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwenye Mkutano wa hadhara uliohusisha kamati ya mawaziri nane wa kisekta na Wananchi wa eneo la Kapunga-Mbarali Mbeya leo Januari 17 mwaka huu.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Naibu Waziri Mavunde amesema  baada ya maboresho ya Mpaka wenye Tangazo la Serikali GN 28 ya kuangalia upya mipaka yake ambayo itaenda kutengeneza eneo la zaidi ya ekari 91,231 kwajili ya Kilimo, ambapo kazi ya Wizara ya Kilimo itakuwa ni kuwapanga wakulima vizuri kwenye maeneo hayo na kujenga Mabwawa 6 Makubwa pamoja na Skimu za Umwagiliaji 8 za kisasa.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi Wizara ya Kilimo tutakwenda kuwapanga Wakulima vizuri, lakini vile vile tutajenga mabwawa makubwa 6 pamoja na skimu 8 za kisasa, ambazo ziahakikisha kuwa maji yanarudi mtoni kwenye njia yake ya asili na hivyo kuchangia katika uwekezaji mkubwa wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa La Nyerere”, alisema Mavunde.

Hata hivyo Wizara ya Kilimo kwa kufuata maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Dkt. Samia Suluhu Hassan* itaweka Mfumo wa Mashamba Makubwa ‘Block Farming System’ kwenye maeneo hayo, pamoja na uwekaji wa  miundombini rafiki kwajili ya Mifugo (`Cattle trough`) katika Mabwawa 14  Nchini, ambayo mabwawa hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji Mita za ujazo 131, 535,000, na kuondoa adha ya mifugo kukosa maji hivyo kutatua migogoro ya Wakulima na Wafugaji Nchini.

Aidha Wizara ya Kilimo imeishukuru Kamati ya Mawaziri nane wa Kisekta kwa mapendekezo yaliyo wasilishwa ya marekebisho ya mipaka yenye tangazo la serikali GN 28.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi Wizara ya Kilimo Tunashukuru sana mapendekezo yaliyowasilishwa ya marekebisho ya mpaka wenye tangazo la Serikali GN 28 ambayo yanakwenda kutengeneza eneo la ukubwa wa zaidi ya hekari 91,231 kwajili ya Kilimo”, alisema Mavunde.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza kuwa wananchi wapewe muda wa kumalizia shughuli zao za Kilimo kabla ya kuondolewa, na kuitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha kwamba inawapanga wakulima vizuri na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya kilimo cja uhakika.

Naye Waziri wa Ardhi Dkt. Angeline Mabula ,ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri 8 wa kisekta amesema kuwa Serikali itachukua hatua za makusudi za kupima maeneo hayo na kuwapatia hati miliki wananchi hao kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara uliohusisha Barala za Mawaziri nane wa Kisekta pamoja na Wananchi wa eneo la Kapunga-Mbarali Mbeya Januari 17 mwaka huu.
Wananchi wa eneo la Kapunga-Mbarali Mbeya wakishangilia maneno ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitoa kauli ya kumaliza Mgogoro wa Ardhi kwenye eneo hiloJanuari 17 mwaka huu.