Skip to main content
Habari na Matukio

Serikali Yaongeza Idadi ya Maafisa Ugani

Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Wizara Kilimo Chakula na Ushirika Bibi Anne Assenga amesema katika msimu wa kilimo wa 2014/2015 Serikali imefanikiwa kuongeza idadi ya Maafisa Ugani na kufikia 11,073 walioajiriwa ikilinganishwa na lengo la kufikia Maafisa Ugani 15,082 ifikapo mwaka 2020.

Bibi Assenga alibainisha hayo wakati akiongea na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, ofisini kwake hivi karibuni na kuongeza kuwa lengo la Serikali ni kuwa na Maafisa Ugani katika kila kata na Kijiji.

Bibi Assenga aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikiongeza idadi ya wanafunzi katika Vyuo vya Kilimo na kwa sababu hiyo Maafisa Ugani wamekuwa wakiongezeka kila mwaka. Hali hiyo imewezesha kila Kata hapa nchini kuwa na Afisa Ugani ukiacha Kata mpya zilizotokana na Serikali kutangaza Mikoa na Wilaya mpya mapema mwaka jana.

Aidha, Bibi Assenga aliongeza kuwa kuongezeka kwa idadi hiyo ya Maafisa Ugani imetokana na Serikali kuweka mkazo wa kusomesha vijana wengi katika Vyuo vya Kilimo sambamba na Vyuo binafsi  kudahiri wanafunzi wengi katika fani ya kilimo.

Bibi Assenga alivitaja Vyuo hivyo binafsi vinavyotoa mafunzo ya fani ya kilimo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kuwa ATI Kilacha (Moshi), St. Maria Gorette College of Agriculture (Iringa), ATI Igabilo (Kagera), College of Agriculture and Natural Resources, CANRE (Dar es Salaam), Mount Sinai Teachers College (Dar es Salaam), Kaole College of Agriculture (Pwani), MAMRE Agriculture and Livestock College (Njombe), Dr. Clement Fumbuka Memorial College (Mwanza) Dabaga Institute of Agriculture (Iringa).

Vyuo vingine ni TRACDI (Dodoma), Mbalizi Polytechnic College (Mbeya) Katavi Polytechnic College (Katavi) na Mbeya Polytechnic College (Mbeya).

Bibi Assenga aliongeza kuwa Wizara inashirikiana na Vyuo binafsi kutoa mafunzo ya kilimo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa kutumia mtaala wa pamoja kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja na kukidhi viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa Idara ya Mafunzo alisema katika muhula mpya wa masomo ulioanza Mwezi Septemba, 2015 katika Vyuo vya Serikali jumla ya wanafunzi 2,596 walidahiriwa ambapo katika idadi hiyo wanaume ni 1,603 na wasichana ni 993.

Katika mwaka wa masomo uliopita jumla ya wanafunzi 453 walidahiriwa, ambapo wanaume walikuwa 291 na wanawake walikuwa 162.  Bibi Assenga alihitimisha kwa kutoa wito kwa vijana wote wanaopenda kujiunga na Vyuo vya Kilimo kujiandaa na muhula mpya ambao maombi yataanza kupokelewa kuanzia Mwezi Mei, 2016.