Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI YARUHUSU WAKULIMA KUUZA MAHINDI NJE YA NCHI

Waziri wa Kilimo Mhe. Charles Tizeba amesema serikali imeruhusu wafanyabiashara na wakulima kuuza nje ya nchi mahindi ili kuimarisha soko na kuchangamsha bei ya zao hilo.

Akiongea ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni Mhe. Dkt.Tizeba amesema serikali imeamua kuwaruhusu wafanya biashara kupeleka  nje ya nchi ili kuwasaidia wakuliama kupata soko lenye manufaa na kuogeza kipato ili waweze kuandaa msimu  mwingine.

Dkt Tizeba amesema Serikali  imefikia hatua hiyo baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa mahindi yaliopo kwa wakulima ni mengi na bei ya mahindi hapa nchini ni ndogo sana.

“Wapo wakulima wana mahindi lakini wanashindwa kuuza kwa kuwa bei ni ndogo hivyo kushindwa kuingia kwenye msimu wa kilimo kwa kukosa pesa za kununua pembejeo”.

Aidha DKT. Tizeba Amewaambia wabunge na watanzania kwa ujumla kwamba awali Kamati ya Kilimo  ilikutana na kujadili suala la mahindi kutokana na unyeti wake, ambapo matokeo yake Serikali kupitia Wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA) ilianza  kununua mahindi kwa wakulima .

Wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA) walianza kununua mahindi katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa  katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma na baadae Rukwa na Songwe ili kuwawezesha wakulima kuingia  katika msimu mwingine wa  kilimo alisisitiza Dkt. Tizeba.

Aidha amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kuacha kuzuia mahindi kutoka nje ya Mikoa yao au Mkoa moja kwenda mwengine ili kuwasaidia watanzania wengine wenye mahitaji hayo.