Skip to main content
Habari na Matukio

Siku 14 zatolewa kwa waliovamia mashamba ya ASA kuondoka

Mkuu wa mkoa wa Morogoro DK KEBWE STEPHEN KEBWE ametoa siku 14 kwa wakuu wote wa wilaya mkoani humo kuhakikisha wanawaondoa mara moja wananchi waliovamia maeneo ya wakala wa mbegu Tanzania  - ASA na kuyaendeleza kwa shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi ya kudumu.

Dk KEBWE ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakulima wa zao la mpunga kutoka wilaya za Malinyi na Ulanga na kusisitiza wakala huo kuyaendeleza maeneo yao ili kuzuia uvamizi huo unaofanywa na wananchi.

Mkuu huyo wa mkoa pia amewataka wakulima kuachana na kilimo cha mazoea ikiwemo kilimo kinachoendelea katika mabonde ya hifadhi na badala yake watumie mbegu bora zinazoendelea kuzalishwa na wakala wa mbegu nchini  ASA kulima katika naeneo yenye miinuko ili kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.

Kwaupande wake kaimu mkurugenzi wa wakala wa mbegu nchini DKT. SOPHIA KASHENGE amesema katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora  kwa wakati na kulima kwa tija ,tayari ASA imezalisha zaidi ya tani 1400 za mbegu za mazao ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuzisambaza kwa wakulima nchini.