Skip to main content
Habari na Matukio
Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA ALIZOCHUKUA WAZIRI WA KILIMO KUFUATIA UBADHIRIFU BODI YA KOROSHO

Dodoma, 17 Novemba, 2019

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA ALIZOCHUKUA WAZIRI WA KILIMO KUFUATIA UBADHIRIFU BODI YA KOROSHO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitoa maelekezo ya kuwa katika msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019 Serikali itanunua korosho zote za Wakulima ili kuwaondoa kwenye kusuasua kwa bei ya korosho.Jumla ya korosho zote zilizokusanywa zilikuwa ni tani 222,561.1 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 732.8.  Korosho hizo zilikuwa za madaraja mawili ambayo ni daraja la kwanza (Standard grade) tani 204,476.1 zenye thamani ya Shilingi 674,522.700 na daraja la pili (Under grade) tani 18,084.9 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 47,744,294,400.  Hadi sasa Serikali tayari imelipa kwa wakulima jumla ya Shilingi Bilioni 707.8 sawa na tania 217,786 za korosho ghafi.

Aidha,hivi karibu Mhe.Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Fedha kutoa Shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kuwalipa wakulima na watoa huduma wengine waliokuwa wanadai malipo yao ya korosho msimu wa 2018/2019.

Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga leo ameongea na waandishi wa habari kuelezea sababu za kutokamilisha zoezi la kuwalipa wakulima hao.Amesema sababu zifuatazo zimechangia ;Kwanza; kuna udanganyifu mkubwa ambao umefanywa na Viongozi wa Vyama vya Msingi katika mkoa wa Pwani. Mfano Chama cha Msingi cha (Sanga Sanga AMCOS) katika msimu uliopita; walikusanya kilo 212 tu lakini kwenye hesabu imeonekana walifanya udanganyifu na kuongeza kilo Elfu 7,000.  Aidha, walitoa taarifa ya uongo kuhusu uwepo wa korosho za daraja la kwanza za kilo 244 badala ya daraja la pili, udanganyifu huo, ulisababisha Serikali kulipa zaidi ya shilingi Milioni 222,328,867 kwenye Chama hicho cha Msingi (Sanga Sanga AMCOS).

Waziri Hasunga amesema pia katika mkoani Mtwara, wilaya ya Tandahimba.  Timu ya Uhakiki ya Wizara iligundua malipo hewa ya Shilingi Bilioni 1.6. Kutokana na mapungufu hayo, Waziri wa Kilimo ameamua kuunda Timu ya Uchunguzi ya watu watano (5) kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa mwenendo mzima wa biashara ya korosho kwa msimu wa 2018/2019.  Timu hiyo imepewa hadi tarehe 15 Januari, 2020 iwe imekamilisha kazi na kuwasilisha ripoti.

Mhe .Hasunga ametaja majukumu ya timu hiyo ya uchunguzi kuwa ni kwanza, kuhakiki majina ya Wakulima kutoka kwenye Vyama vya Msingi, kwenda Vyama Vikuu na baadae Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwenda kwenye mfumo wa malipo ya Benki ili kubaini fedha walizolipwa Wakulima zililipwa kupitia, akaunti zao.

Pili, kuchunguza kama kulikuwa na unyaufu kwenye korosho zote, zilizonunuliwa kwenye msimu wa 2018/2019 na kama unyaufu ulikuwepo, ulikuwa ni wa kiwango gani ili Serikali itoe taarifa inayoendana na uhalisia.

Tatu,kuchunguza matumizi mabaya ya Shilingi Bilioni 53.2 zilizokuwa za Mfuko wa Wakfu wa Maendeleo ya zao la Korosho (Cashewnut Development Trust Fund - CDTF) zilizokuwa zikisimamiwa na Bodi ya Korosho.  Fedha hizo kazi yake ilikuwa kuendeleza tasnia ya korosho kwa kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho na ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho.  Viwanda hivyo vilikuwa vijengwe eneo la Mkinga (Tanga), Mkuranga (Pwani) na Tunduru (Ruvuma).

Waziri Hasunga ameeleza kusikitishwa kwake kuona Bodi ya Korosho ilishindwa kutekeleza majukumu hayo ya kujenga viwanda hivyo na ghala badala yake fedha hizo zilitumika kinyume na makusudio. Jambo baya zaidi kuna viashiria ambavyo vinatia shaka na kutoa tahadhari ya kufanyika kwa haraka kwa uchunguzi wa kina wa namna fedha hizo zilivyotumika. Viashiria hivyo ni pamoja na matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 600 zilizotumika kwa ajili ya kulipia gharama za uandaaji wa mikutano ya Wadau, pamoja na malipo ya pembejeo kiasi cha zaidi ya Bilioni 28 na malipo kwa Watoa huduma (Wauzaji wa magunia). Malipo ya shilingi Bilioni 12 ambayo yameonekana, yalishalipwa kwa watoa huduma hao.Malipo mengine tunayotilia mashaka ni pamoja na Bodi ya Korosho kuvilipa Vyama Vikuu vya TANECU Bilioni 1.8, CORECU Bilioni 2.1 kwa maelezo kuwa hayo ni madai ya miaka iliyopita ambapo Bodi ya Korosho ilikuwa ikidaiwa.

Mwisho Mhe Waziri wa Kilimo amemwelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uhakiki na uchunguzi ili kuangalia namna kiasi cha fedha cha shilingi Bilioni 53.2 zilivyotumika katika Bodi ya Korosho na kama itabainika, wale wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo za umma wachukuliwe hatua kwa mujibu ya sheria za nchi.

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo