Skip to main content
Habari na Matukio

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wanahabari, nimewaita leo hapa ili niweze kuzungumza nanyi na umma wa Watanzania wote kuhusiana na Maendeleo ya vyama vya ushirika hapa nchini.

UTANGULIZI

Ndugu Wanahabari,

Kama sote tunavyofahamu kuwa Chama cha Ushirika ni chama kinachoanzishwa kwa hiari ya watu wenyewe chenye malengo mahsusi ya kuwahudumia wanachama wake. Lengo kuu ni kuwaunganisha wanachama wake ili wawe na msimamo wa pamoja juu ya utatuzi wa tatizo au kufanya shughuli fulani ya kiuchumi na kijamii inayolenga katika kuwabadilisha maisha yao kiuchumi au kijamii. Kwa kuzingatia sheria ya ushirika, ushirika ni chombo binafsi na Mwanachama yupo huru kujiunga au kutoka kwa kadri ya uamuzi wa mwanachama mwenyewe kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu walizojiwekea wenyewe.

Ndugu Wanahabari,

Vyama vya Ushirika vinaanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013. Kwa mujibu wa sheria hiyo ya ushirika, Chama cha Ushirika ni Taasisi inayotakiwa ianze na kufanya kile kilichokusudiwa kwa mujibu wa katiba yake na kanuni na miongozo ya ushirika.

Ndugu Wanahabari,

Kutokana na maendeleo ya ushirika nchini na kwa mujibu wa daftari la kudumu la vyama vya ushirika (rejista), hadi hivi leo tarehe 05 Mei, 2020 kuna jumla ya vyama vya ushirika 11,626 vyenye jumla ya wanachama 5,880,736. Mchanganuo wa vyama hivyo ni kama ifuatavyo; vyama vya ushirika wa mazao – AMCOS (3,835), Nyuki (56), Walaji (98), Uvuvi (121), Nyumba (31), Viwanda (91), Umwagiliaji (82), Ufugaji (238), Madini (98), SACCOS (6,178), Huduma (121), Usafirishaji (17), Vyama Vikuu (56), Miradi ya pamoja (40), Benki (1) na Vingine (563).

Ndugu Wanahabari,

Kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013, majukumu ya Chama cha Ushirika ni kama yafuatayo;

 

                  i.      Kuinua hali ya maisha ya wanachama wake;

 

                 ii.      Kutoa huduma kwa wanachama wake zikiwemo mahitaji ya pembejeo za kilimo, kukusanya, kusindika na kutafuta masoko ya bidhaa za wanachama wake;

 

                iii.      Kutoa taarifa zinazohusiana na shughuli zake kwa mujibu wa sheria na

 

               iv.      Kutoa huduma kwa Vyama vya Msingi kama ilivyoainishwa kwenye Masharti ya Chama.

Ndugu Wanahabari,

Viongozi wa Ushirika wana wajibu wa kuhakikisha kuwa Vyama vya ushirika vinatekeleza majukumu kwa uwazi, haki na usawa ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya ushirika. Kazi ya Kiongozi ni kulinda maslahi ya Wanachama na mali zao.

Ndugu Wanahabari,

Hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika ambao wamekuwa wanatenda kinyume na matarajio ya wanachama wao, kinyume na sheria ya ushirika, kanuni na miongozo yake. Hivyo, tutaendelea kujenga uwezo wa vyama hivyo kwa kupitia upya sheria ya ushirika, namna bora ya kusimamia na kuboresha sifa za kuwapata viongozi wake. Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka au watakaoenda tofauti na sheria, kanuni na miongozo ya ushirika.

MAFANIKIO MAKUU YA USHIRIKA

Ndugu Wanahabari,

Ushirika umefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kuwahudumia wananchi kwa sasa, kama unavyojidhirisha katika zao la Korosho, Tumbaku, Kahawa, Pamba n.k. Aidha, idadi ya vyama vya ushirika imeongezeka kutoka vyama 7,394 Mwaka 2015/16 hadi kufikia vyama 11,626 Mwezi Aprili, 2020. Pia, thamani ya mikopo inayotolewa na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS)   imeongezeka kutoka trilioni 1.3 Desemba, 2018 hadi kufikia trilioni 1.5 Machi, 2020. Vilevile, thamani ya hisa, akiba na amana imeongezeka kutoka shilingi bilioni 654 Desemba, 2018 hadi kufikia bilioni 819 Machi, 2020. Mafanikio haya na mengine mengi ni matokeo ya jitihada za Serikali za kuimarisha ukaguzi na udhibiti wa vyama vya ushirika nchini kwa lengo la kuakisi dhana ya uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika kuendeleza ushirika nchini.

Ndugu Wanahabari,

Kama mtakumbuka mnamo tarehe 05 Januari, 2020 nilitangaza kusudio la Serikali la kuvifuta baadhi ya vyama vya ushirika nchini ambavyo vilikuwa havifanyi kazi, ama kutotekeleza majukumu yake ya msingi na vingine hewa. Kwa mujibu wa kifungu cha 100 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya Mwaka 2013, na Kanuni ya 26 ya Kanuni za Vyama vya Ushirika za Mwaka 2015, tulitoa notisi ya siku 90 ya kusudio la kuvifuta vyama 3,436 kutoka katika daftari (rejista) la Vyama vya ushirika.

Ndugu Wanahabari,

Katika notisi hiyo ya siku 90, Serikali ilitoa nafasi kwa Mtu, Chama au Taasisi yoyote yenye pingamizi kuhusu kufutwa kwa Vyama hivyo vya Ushirika vilivyoorodheshwa, kuwasilisha pingamizi yake kupitia Ofisi za Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa. Notisi hiyo iliisha tarehe 17 Aprili 2020 na hivyo kuniwezesha kuvifuta vyama ambavyo havijajitokeza kupinga. 

Ndugu Wanahabari,

Kabla ya muda wa kutoa pingamizi kumalizika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ilipokea jumla ya mapingamizi 88, ambayo yalichambuliwa na kufikiwa uamuzi wake kwa  kuzingatia maoni ya Warajis Wasaidizi wa Mikoa husika. Kutokana na hali hiyo, Serikali imejiridhisha na kukubaliana na mapingamizi hayo ya kutokufutwa kwa Vyama hivyo 88 na kwamba Warajis Wasaidizi wa Mikoa watawajibika kusimamia Vyama hivyo ili kuhakikisha kuwa vinaendeshwa kulingana na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013.

Ndugu Wanahabari,

Hivyo basi ninatangaza kuvifuta Rasmi vyama vya Ushirika 3,348 ambavyo vingi ni hewa, na vipo katika mchanganuo ufuatao:  SACCOS (2,513), AMCOS (229), Mifugo (77), Vyama vya walaji (27), Vyama vya huduma (70), Vyama vya ufugaji nyuki (15), nyumba (9), madini (22), Viwanda (79), uvuvi (32), umwagiliaji (31) na vinginevyo (244). Kufuatia kufutwa kwa vyama vya ushirika 3,348 kwa sasa Rejista ya vyama vya ushirika nchini itabaki na jumla ya vyama vya Ushirika 8,611.

Ndugu Wanahabari,

Orodha inayoonesha idadi ya vyama vya ushirika vinavyobaki kwa kila Mkoa nitawapatia baada ya kutoa taarifa hii. Aidha, orodha kamili ya vyama hivyo vinavyovutwa na vinavyobaki kwa kila Mkoa na aina ya chama itapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Kilimo www.kilimo.go.tz na tovuti ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) www.ushirika.go.tz punde baada ya kumaliza kutoa taarifa hii.

Ndugu Wanahabari,

Pamoja na kufuta vyama hivyo, ili kuimarisha mwenendo wa vyama vya ushirika nchini ninatoa maelekezo yafuatayo;

 

     i.        Vyama vianzishwe kwakuzingatia matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013 ikiwemo vigezo katika kuanzisha Chama cha Ushirika kama vile kuzingatia uhai wa kiuchumi, Chama kuwa endelevu kwa kumudu gharama za uendeshaji na kuzingatia mahitaji ya Wanachama wenyewe.

 

    ii.        Zoezi la kufuta Vyama litakuwa endelevu kwa Vyama vya Ushirika vitakavyoshindwa kutekeleza majukumu ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika.

 

  iii.        Natoa  wito kwa Wakulima/Wanachama wanaovitumia Vyama vya Ushirika nchini kufungua Akaunti Benki ili Mkulima kujihakikishia malipo yake. Hii itakuwa mojawapo ya suluhu kwa udanganyifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika wasio waaminifu wakati wa malipo.

 

  iv.        Kuhusu zuio la mikusanyiko ambalo lilitolewa na Serikali kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID - 19) unaosababishwa na virusi vya CORONA, Zuio la Mikutano yote na mikusanyiko inayohusisha Vyama vya Ushirika litaendelea. Aidha, kutokana na zuio hilo kuendelea, Bodi za Vyama vya Ushirika zinaelekezwa kuomba kibali cha kukasimiwa madaraka ya Mkutano Mkuu kwa Mrajis ili ziweze kupitisha baadhi ya maamuzi ikiwemo bajeti za Vyama vyao kwa niaba ya Mkutano Mkuu wa wanachama wote.

2.0 MFUMO WA UNUNUZI WA MAZAO NCHI NZIMA

Serikali ya awamu ya tano tuliamua kuwa, njia pekee ya kumkomboa Mwananchi ni kupitia ushirika.  Hivyo, tunataka wananchi wajiunge kwenye ushirika ili wanufaike na ushirika.  Wananchi wakiuza kwa pamoja ni rahisi kupata bei nzuri. Hata hivyo, kumetokea malalamiko mengi katika baadhi ya Mikoa kuwa wananchi wananyanyasika  sana na mfumo wa Vyama vya Ushirika  na Stakabadhi Ghalani.

Ndugu Wanahabari, ili mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kufanyika sawasawa mambo yafuatayo lazima yazingatiwe:-

 

i.                 Kuwepo kwa chama cha msingi kilichosajiliwa katika kijiji husika;

ii.                Kuwepo na ghala lililosajiliwa na Bodi ya Maghala;

iii.               Kuwepo kwa mfumo wa kufanya minada  kwa njia ya ushirika;

iv.               Kuwepo kwa wanunuzi wa kununua kwa minada.

 

Ndugu Wanahabari, siyo kila zao lazima kuuzwa kwa stakabadhi ghalani.  Kwa mfano karanga, choroko n.k.   ni muhimu kuzingatia ukubwa wa mzigo na upatikanaji wa wafanyabiashara

Ndugu wanahabari, kutokana na changamoto hizo tunaagiza mambo yafuayo kufanyika:

(i)                 Kuhakikisha kuwa katika kila kijiji kunakuwa na soko la awali  ambalo wananchi watauza mazao yao;

(ii)                Kutakuwa na soko la upili ambalo wananchi,  vyama vya ushirika na wafanyabiashara wa ndani wataruhusiwa kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa nje;

 

Ndugu wanahabari, tunaomba ifahamike kuwa kwa sasa hatukusudii kufunga mipaka yetu kwani ni vizuri wananchi wakaruhusiwa kuuza wanapotaka.

Asanteni sana kwa kunisikiliza