Skip to main content
Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari Kuhusu Utatuzi Wa Mgogoro Wa Wakulima Wa Miwa Kilombero

Bodi ya Sukari Tanzania imefuatilia na kubaini chanzo cha malalamiko ya wakulima wa miwa wanaozunguka Kiwanda cha Sukari cha Kilombelo (ILOVO). 

Akizungumza katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Sukari Tanzania Bwana Henry Semwanza alisema kuwa, chanzo cha malalamiko yanatokana na kiwanda kuharibika bila kutarajia na kusimamisha uzalishaji kuanzia tarehe 14 hadi 18 Novemba 2015. 

Hali hiyo ilisababisha miwa ya wakulima ambayo ilikuwa imekatwa kuharibika na hivyo kukosa sifa ya kuchukuliwa na kiwanda kwa ajili ya usindikaji. 

Bwana Semwanza aliongeza kuwa hali hiyo ilisababisha tani 250 za miwa kutoruhusiwa kuingia kiwandani kwa vile zilishapita zaidi ya siku tano tangu miwa ilipochomwa. 

“Miwa hiyo ilichomwa tangu tarehe 14 Novemba 2015 siku ambayo kiwanda kiliharibika, na kilipotengamaa zilikuwa zimeshapita siku tisa, hivyo miwa hiyo kukosa sifa na ubora unaokubalika, na hivyo ikazuiliwa kuingia kiwandani” 

Akizungumzia utekelezaji wa mkataba wa ugavi wa miwa baina ya Kampuni na Vyama vya Wakulima, Bwana Semwanza alibainisha kuwa Kifungu cha 5.2.3.3 cha mkataba huo kinasisitiza kutokuikubali miwa ambayo kiwango cha ubora wake uko chini ya asilimia 80 au miwa iliyopitisha siku tano tangu ilipochomwa kwa mujibu wa kifungu cha 5.2.3.4. 

Ili kupunguza hasara inayoweza kutokea kwa wakulima, Bwana Semwanza aliwakumbusha wakulima na wamiliki wa kiwanda kuzingatia taratibu za uvunaji wa miwa. 

“ninatoa wito kwa wakulima kupitia vyama vyao kuzingatia taratibu za uvunaji kwakuwa imedhihirika pasipo shaka kuwa baadhi wamekuwa wanavuna miwa mingi zaidi ya mgao wao wa siku, mambo haya yasipozingatiwa yanaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima ” Bwana Semwanza alibainisha katika taarifa yake. 

Aidha, alisisitiza kuwa kamati iliyoundwa chini ya mkataba wa ugavi wa miwa inayojumuisha wakulima na uongozi wa Kiwanda na ambayo hukutana kila siku iendelee kuwa msingi wa kuamua kiasi cha miwa inayotakiwa kuvunwa na kupelekwa kiwandani katika siku inayofuata. 

Semwanza aliongeza kuwa Bodi yake inaendelea kufuatilia utekelezaji wa makubaliano kati ya kiwanda na wakulima, na haitasita kuchukua hatua sitahiki kwa upande utakao kiuka ili kutatua migogoro inayoweza kuzuilika kwa haraka.

Semwanza alisisitza kuwa kwa sasa hali ni shwali ambapo uvunaji na upokeaji wa miwa kiwandani unaendelea kama kawaida na wakulima wameongezewa mgawo wa miwa inayotakiwa kuingizwa kiwandani kila siku. 

“hali ya uvunaji inaendelea kama kawaida na mgao wa wakulima kuingiza miwa yao kiwandani umeongezwa kwa zaidi ya asilimia 50; ili kuhakikisha miwa yote ya wakulima wanaozunguka kiwanda cha Kilombero inavuwa” 

Bodi ya Sukari Tanzania inashirikiana kwa karibu na uongozi wa mkoa na Wilaya ili kushughulikia migogoro isiyo ya lazima. Alihitimisha Bwana Semwanza.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex, 
1 Mtaa wa Kilimo 15471
DAR ES SALAAM