Skip to main content
Habari na Matukio

TANIPAC Yadhamiria kuondoa Sumukuvu

Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa kudhibiti Sumukuvu nchini ( TANIPAC) inatarajia kujenga maghala (14) ambayo yatatumika  kuhifadhia mahindi lengo likiwa ni  kuondoa tatizo la  sumukuvu kwenye mazao ya nafaka na mafuta.

Sumukuvu inaathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga kutokana na namna ya na wakati wa kuvuna na kuhifadhi  ambapo  unyevuunyevu unaopatikana  kwenye mazao husababisha uotaji wa fangasi  na kuwa chanzo cha  sumukuvu.

Mratibu  wa mradi ,Clepine Josephat alisema kwamba mradi huo una sehemu kuu tatu,Kujenga miundo mbinu, Kujenga uelewa na Uratibu. Katika ujenzi wa miundo mbinu  yatajengwa maghala ambayo yatasaidia kuhifadhi mahindi. Mradi huu utahusisha pia  kujenga uelewa kwa wakulima namna ya kuhifadhi mazao baada ya kuvuna ili kudhibiti sumukuvu kwenye mazao ya nafaka.

Clepine aliyasema hayo wakati alipokuwa akikagua maeneo ambayo yamechaguliwa kwaajili ya ujenzi wa maghala  katika mikoa ya Pwani, Manyara, Dodoma  na  Zanzibar.

Katika mkoa wa Manyara ,mradi unatekelezwa kata ya Gallapo, Kijiji cha Endanoga, ambapo wanakijiji wameupokea mradi huo  vizuri  na wametoa hekta 3 kwa ajili ya ujenzi wa maghala  yatakayotumika  kuhifadhia nafaka kwa ubora na kiwango ili kuondoa sumukuvu.

“Tutajenga ghala kubwa hapa na pia tutatoa elimu jinsi ya uhifadhi wa mahindi baada ya kuvuna,kijiji chenu kina tatizo la sumukuvu na tumepoteza  baadhi ya wenzetu kutokana na athari ya sumukuvu hivyo uwepo wa ghala hilo ni muhimu sana kwa kutunza mazao yetu” alisema clepine

Aidha,Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)  Salum Ramadhan alisema mradi unahusisha ufuatiliaji kuona endapo malengo ya kusaidia wakulima kuelewa tatizo la sumukuvu na jinsi ya kutatua yanafikiwa na ndio maana ameshiriki ziara hiyo.

Mradi wa TANIPAC  unalenga utakapo kamilika kuwezesha jamii kutumia njia sahihi na za kisasa za uhifadhi wa nafaka hususan mahindi kutokana na sumukuvu.

“Tatizo la sumukuvu linasababisha mazao ya wakulima kukosa bei nzuri kwenye masoko, hii hupelekea mkulima kupata hasara” alisema Clepine

Clepine alisema kuwa mradi utahakikisha elimu kwa wataalam wa kilimo vijijini inafikishwa hususan kupitia vyombo vya habari.