TANIPAC YAJA NA MKAKATI WA KUDHIBITI SUMUKUVU.
Na. Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Serikali imesema imekusudia kudhibiti madhara ya sumukuvu katika mfumo wa Chakula kupitia mradi wa Udhibiti wa sumukuvu (TANIPAC) katika mazao ya mahindi na karanga nchini unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo. Mradi huo unalenga udhibiti wa sumukuvu katika hatua za uzalishaji, uvunaji, udhibiti wa kibailojia, teknolojia baada ya kuvuna, ukaushaji, uhifadhi na kutoa elimu ya kuhamasisha wadau muhimu.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Alfasafe) kwenye vyakula uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha jana (04 Novemba,2019) Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga alisema mradi huo utakuwa na manufaa katika kuifanya jamii kuwa na lishe bora na mazao salama.
“Tanzania imeanzisha Kamati Jumuishi ya Uendeshaji inayohusisha sekta na taaluma kutoka taasisi mbalimbali chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Kilimo ambayo ina mamlaka ya kusimamia masuala yote yanayohusu sumukuvu.” Alisema Hasunga
Waziri Hasunga aliongeza kusema ushirikiano wa kiutafiti kati ya sekta binafsi na watunga sera, ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kilimo nchini.
"Napenda kuwahakikishia utayari wa Wizara yangu katika kuyatumia maazimio mtakayokubaliana katika mkutano huu.” Alisisitiza Waziri wa Kilimo na kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania, inatilia maanani na inaunga mkono hatua zinazochukuliwa katika kuhimiza biashara ya chakula salama, usalama wa chakula na lishe.
Waziri Hasunga amesema kuwa kutokana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka 2017, Tanzania inaongoza katika uzalishaji wa mahindi na karanga katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuzalisha tani milioni 6 na tani milioni moja mtawalia.
Amesema, Pamoja na mafanikio hayo, Serikali inatambua kuwa, tatizo la sumukuvu linakabiri mazao haya hivyo linahatarisha usalama wa chakula na kuwa kikwazo cha biashara ya mazao hayo kwa nchi jirani na Tanzania.
Mkutano huo ambao umewaweka pamoja watafiti, wafanyabiashara, watunga sera na wadau wa maendeleo, ambao unalenga kupanga mikakati ya kuongeza kasi ya matumizi ya kinga ya sumukuvu (Alfasafe), na kukabili sumukuvu barani Afrika, unadhihirisha mabadiliko chanya ya kimtazamo tunayoyahitaji.
Katika hatua nyingine,Waziri Hasunga alisemaTanzania kwa sasa inatekeleza Awamu ya Pili Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo (ASDP II) yenye lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo kuwa na kilimo chenye tija na kibiashara, pamoja na kukuza uchumi wa wakulima wadogo na kuboresha maisha, uhakika wa chakula na lishe bora.
Uhakika wa chakula na lishe ni muhimilia mbao ni muhimu wa ASDP II katika kufikia malengo hayo, uwekezaji katika utafiti wa kilimo ni muhimu katika kuleta matokeo kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.
MWISHO