Skip to main content
Habari na Matukio

TANZANIA INA UTOSHELEVU WA CHAKULA-WAZIRI HASUNGA

Dodoma

Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula ili watu wake wawe na nguvu ya kufanya kazi kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025

Kauli hii ya serikali imetolewa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha nne cha Menejimenti ya wizara kinachojumuisha wakurugenzi,wakuu wa taasisi na bodi za mazao nchini.

Waziri Hasunga amesema kwa miaka mitatu  sasa serikali ya imeendelea kuhakikisha nchi inazalisha mazao mengi na ya kutosha ya chakula kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wizara ya kilimo na taasisi zake.

“Nchi yetu ina utoshelevu wa chakula asilimia 119 mwaka 2019 ambapo tani milioni 16.4 za mazao ya chakula zilizalishwa nchini na zinatumika msimu huu tunapoendelea na msimu wa kilimo ” alisema Waziri wa Kilimo

Alibainisha kuwa uzalishaji huo wa mazao ya chakula ulishuka ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo nchi ilizalisha tani milioni 16.8  hali inayoifanya nchi kuwa na chakula cha kutosha

“Kila mtu lazima ale chakula kwa wingi,hivyo  jukumu la wizara ya kilimo ni kuhakikisha nchi inazalisha zaidi  ili wananchi wawaze kuwa na nguvu za kufanya kazi na kuzalisha malighafi za viwandani” Hasunga

Amewapongeza wakulima nchini kwa kuitikia wito na maelekezo ya serikali katika kuhakikisha uzalishaji nchini unaendelea kuongezeka hususan kwenye mazao ya chakula na biashara.

Pamoja na utoshelevu huo,waziri wa kilimo amesema kuna mikoa nane (8) yenye halmashauri 44 ina upungufu kidogo wa chakula  ambapo serikali tayari imeandaa mpango wa kupeleka chakula toka hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kunusuru hali hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameigiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha inaharakisha upatikanaji na usambazaji wa mbolea aina ya UREA ambayo imeadimika kwa wakulima.

“Wiki za karibuni kumetokea upungufu wa mbolea ya UREA hali inayosababisha kupanda bei na wakulima wengi kulalamika mazao yao kukosa mbolea hii muhimu” Waziri wa kilimo alisema

Waziri Hasunga ameitaja mikoa ya Ruvuma,Mbeya,Songwe na Njombe kuwa ni maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula lakini kwa sasa mbolea ya UREA imeadimika.

Ameitaka Menejimementi ya TFRA kuchukua hatua za  haraka  za usimamizi wa mfumo wa ununuzi mbolea wa pamoja ili wakulima wapate mbolea kwa bei nafuua na kwa wakati .

MWISHO

Imeandaliwa na

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

DODOMA