Skip to main content
Habari na Matukio

Tanzania yaweka wazi mikakati kuinua kilimo cha zabibu

Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikapunguza uagizaji wa mchuzi wa zabibu (wine) kutoka nje ya nchi baada ya Serikali kuainisha mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo ikiwemo kutumia miche bora ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, Tanzania hutumia Dola za Marekani milioni 6 (Sh19.5 bilioni) kila mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 10 za mchuzi wa zabibu nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya ndani. 

Mahitaji ya mchuzi wa zabibu kwa mwaka ni wastani wa lita milioni 15 ambapo uzalishaji wa ndani ni wastani wa lita milioni 5. 

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuinua uzalishaji zao la zabibu utakaosaidia bidhaa zake kusindikwa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi. 
 

“Sasa Serikali imeliingiza zao la zabibu kuwa moja ya mazao ya kimkakati ambayo yamepewa kipaumbele katika kuendelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi,” amesema Bashe leo Agosti 31 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde. 

Mavunde alikuwa anataka kufahamu mikakati ya Serikali ya kukuza zao hilo mkoani Dodoma.

“Mikakati ni kuhakikisha upatikanaji wa miche bora kupitia TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania) na halmashauri za wilaya husika, kuimarisha huduma za ugani za zao la zabibu, kuongeza wigo wa soko kutoka wastani asilimia 65 hadi asilimia 85,” amesema Bashe. 

Pia kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya zabibu, kufufua na kuanzisha mashamba makubwa ya zabibu na kutenga na kulinda ardhi kwa ajili ya kilimo cha zao hilo.

“Serikali imefufua shamba la Chinangali II lenye ukubwa wa ekari 602 lilipo wilaya ya Chamwino kwa kukarabati bwawa la maji na visima vilivyopo shambani,” amesema naibu waziri huyo.

Kutokana na mikakati hiyo, Serikali inakusudia kuongeza tija ya uzalishaji wa zabibu kutoka  tani 6.25 za sasa kwa hekta hadi kufika tani 30 ifikapo 2025.

Uzalishaji wa zabibu kwa sasa nchini Tanzania ni wastani wa tani 16,000 kwa mwaka ukilinganisha na uwezo uliopo wa kuzalisha tani 150,000 kwa mwaka. 

Hii inaweza kuwa fursa kwa wakulima wakiwemo wa Mkoa wa Dodoma kuongeza uzalisha ili kufaidika na soko la ndani la zao hilo.