Skip to main content
Habari na Matukio

Tathmini ya Mashine za Kuvunia Mpunga Yafanyika

Wataalamu 20 kutoka Idara ya Zana za Kilimo  wameanza kufanya tathmini ya mashine mbalimbali za kuvunia mpunga kufuatia mafunzo yaliyotolewa awali juu ya matumizi na uendeshaji lengo likiwa ni kutatua vikwazo vilivyojitokeza wakati wa matumizi na uendeshaji wake. Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Zana za Kilimo Eng. Rajabu Mtunze alipozungumza  na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali ofisini kwake, hivi karibuni.

Wilaya zinazofanyiwa tathmini na  wataalam hao wa zana za kilimo ni Mbarali Mkoa wa Mbeya, Songea, Mkoa wa Ruvuma;  Mvomelo na Kilosa katika Mkoa wa Morogoro. Eng.  Mtunze alizitaja Wilaya nyingine kuwa ni Iringa Vijijini, Mkoa wa Iringa; Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Korogwe Mkoa wa Tanga.

Wilaya zilizopata mafunzo hayo kwa Mkoa wa Kilimanjaro ni Mwanga na Hai wakati katika Mkoa wa  Arusha ni Arumeru na Babati katika Mkoa wa Manyara.

Mashine zitakazofanyiwa tathmini ni ‘Combine Harvester’ ambazo zina uwezo wa kuvuna, kukoboa na kufungasha mpunga katika mifuko. Mashine nyingine ni za kupandia ‘Leaper”. Mashine nyingine ni za kukata na kupiga punga ‘Thresher’.

 “Wataalamu hao pia watatoa mafunzo kwa waendeshaji wapya wa mashine hizo baada ya wengine kumaliza mikataba yao na pia watafuatilia ujenzi wa majengo ya kuwekea mashine za kukoboa na kupanga madaraja ya mpunga kuhakikisha yanakamilika ili mashine hizo zianze kufanya kazi”, alibainisha Eng. Ntunze.