Skip to main content

UMWAGILIAJI UTAONGEZA TIJA NA UZALISHAJI WA ZAO LA CHAI - PROF. MKENDA

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ili kukabiliana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa zao la chai nchini wizara yake itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa miche bora ili zao la chai lilimwe kwenye maeneo mengi nchini

Amesema wizara ya kilimo itahakikisha inatumia wataalaam wake wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na taasisi za fedha kupata mitaji itakayowekezwa kwenye kujenga miundombinu muhimu ya umwagiliaji ili zao la chai ambalo linastawi kwenye wilaya zaidi ya kumi na mbili nchini lilimwe na kuvunwa mwaka mzima.

“Tutafuta fedha toka kwa wadau wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) ili tujenge miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa chai hatua itakayohakikisha tunaongeza uzalishaji wa majani mabichi ya chai mwaka mzima  badala ya kutegemea mvua” alisema Prof. Mkenda.

Waziri wa Kilimo ametoa kauli hiyo jana (11.03.2021)wakati alipotembelea mashamba ya wakulima wadogo wa chai kijiji cha Lwanga wilaya ya Njombe wanaoratibiwa na kampuni ya huduma kwa wakulima Wadogo Njombe (NOSC).

Waziri Mkenda aliogeza kusema ili kukuza uzalishaji wa zao la chai suala la kutumia teknolojia ya umwagiliaji na matumizi ya miche bora ni muhimu na kuwa wizara itatafuta wadau kusaidia wakulima wadogo kumwagilia mashamba yao .

Prof. Mkenda aliwasihi wanachama wa NOSC kupanua mashamba yao kwani wana uhakika wa soko kwenye kiwanda cha kampuni ya Unilever (UTT) inayonunua majani mabichi ya chai ya wakulima hao.

Aidha, Waziri huyo wa kilimo aliagiza bodi ya chai na Taasisi utafiti wa zao la chai (TRIT) kuzalisha miche bora ya chai na kuigawa kwa wakulima ili wapanue mashamba mapya na kuziba mapengo kwenye mashamba ya zamani.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe (Njombe Outgrowers Services Company –NOSC) Meneja Mkuu wake John Mhagama alisema wamefanikiwa kuanzisha mashamba mapya ya chai hekta 1,345 kati ya kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019.

Aliongeza kusema katika mwaka 2020/2021 wamepanda hekta 275 hivyo kupelekea kufikia jumla ya hekta 1,620 za mashamba mapya ya chai.

Kuhusu kiwango cha uzalishaji chai Mhagama alisema wakulima wadogo wameongeza uzalishaji toka kilo 3,364 za majani mabichi  kwa hekta hadi kilo 5,977 na sasa lengo ni kufikia wastani wa kilo 11,250 endapo miundombinu ya umwagiliaji ikikamilika.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakulima Wadogo wa Chai Phillemon Luhanjo alishukuru serikali kupitia waziri wa kilimo kwa kuwasaidia wakulima kupata huduma za ugani hatua inayokuza ubora wa chai.

“Sisi wakulima wakulima tunafurahi kuiona serikali ikifuatilia utendaji kazi wetu na kututia moyo tuendelee kuhudumia mashamba yetu ya chai .Tutaongeza mashamba mapya ili lengo la nchi lifikiwe “ alisema Mzee Luhanjo ambaye pia ni mkulima wa chai.

Kwa mwaka uzalishaji wa majani mabichi ya chai kwa mujibu wa takwimu za bodi ya chai umefikia tani 32,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima kwenye wilaya zote 12 zinazolima zao hilo nchini.

Ziara hii ya Waziri Mkenda kwa wakulima wadogo wa chai inafuatia kikao cha wadau wa zao la chai kilichofanyika mkoani Njombe juzi chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye aliagiza Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wadau kujua namna ya kutatua kero .

Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
NJOMBE

11.03.2021