Skip to main content
Habari na Matukio

Uzalishaji wa zao la korosho waongezeka

Katibu Mkuu  Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma amesema kuwa Tanzania imeweka rekodi mpya kwa kuzalisha karibu tani  200,000 za korosho katika msimu wa 2014/2015 ukilinganisha na tani 158,000 zilizozalishwa mwaka 2011.

“Kiwango hiki cha uzalishaji ni mafanikio chanya si tu kwa Wanasayansi na  Watafiti lakini pia katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho wakiwemo Maafisa Ugani, Wataalamu wa soko, wasambazaji wa pembejeo na wakulima” alifahamisha Bibi. Kaduma.

Pia Bibi. Kaduma alibainisha kuwa Tanzania ni nchi pekee Barani Afrika ambayo imefanya ugunduzi wa  aina mpya ya mbegu na mbegu chotara za korosho kwa kufuata viwango vya Kimataifa ambapo hadi sasa aina 16 zimeruhusiwa kutumiwa na wakulima na aina 22 zipo katika hatua za mwisho za utafiti. Aina hizo 16 za mbegu za korosho zinatoa mavuno mengi na zina kiwango bora cha punje na  tayari zinalindwa kisheria.

Aidha, Bi.Kaduma aliongeza kuwa Tanzania ni nchi pekee duniani inayouza korosho kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao umechangia kupandisha bei kwa mkulima na kuongeza ubora wa korosho ghafi zinazozalishwa nchini.

 “Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizoweka mfumo wa kuwawezesha Wadau kuchangia maendeleo ya Sekta ya korosho, moja ya mfumo huo ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Wakfu wa  Kuendeleza zao la Korosho ambao ni kiungo muhimu katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho,  kwani unachangia katika shughuli za utafiti,  kusambaza pembejeo kwa wakulima, usindikaji, soko na ubora” alifahamisha Bibi Kaduma katika hotuba yake.

Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho umepiga hatua kubwa kwa kuwawezesha wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa korosho kuwapatia mikopo na pembejeo. 
Nchi zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Kenya, Uganda, Nigeria, Ivory Coast, India, Burkina Faso na China.

Nchi nyingine ni Australia, Algeria, Pakistan, Zimbabwe, Sri Lanka, Cape Verde,  Marshall Island,  Malawi na mwenyeji wa mkutano huo Tanzania.
Mazingira.

Mkutano huo uliofanyika Jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Serena na uliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho na Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Korosho (CIDTF)  na ulibeba  Kaulimbiu  isemayo Korosho kwa Afya, Utajiri na Mazingira.