Skip to main content
Habari na Matukio

VYUO VYA KILIMO VYATAKIWA KUJIENDESHA KIBIASHARA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya amesema wigo mpana uliopo katika sekta ya kilimo kwenye utunzaji wa mazingira na uendelezaji wa viwanda utumike kupunguza utegemezi  wa ajira serikalini kwa wahitimu wa vyuo vya kilimo.

Akiongea  mara alipotembelea Chuo  Cha  Sukari   Cha Taifa (NSI ) kilichopo Kidatu Kilombero mkoa wa Morogoro  Bw .Kusaya amesema  vyuo hivyo vitumie taaluma walizonazo ikiwemo uzalishaji wa mkaa mbadala na karakana zilizopo kwenye vyuo vyote vya kilimo kuongeza taaluma na kuweza kujiajiri pindi wanapohitimu vyuo hivyo.

Amesema kwa kuwa kilimo hakiwezi kutenganishwa na utunzaji wa mazingira na uendelezaji wa viwanda vidogo ni lazima wanafunzi wanapohitimu katika vyuo vya kilimo wawe ni chachu katika kuendeleza viwanda vidogo na utunzaji wa mazingira.

 Aidha, akiongea na mwanafunzi anayejishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala Katibu  Mkuu ameahidi kumkutanisha  Bi. Upendo Emanuel mwanafunzi wa stashahada katika chuo hicho na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na  utengenezaji wa bidhaa hiyo ili kuongeza ujuzi

“Nataka wanafunzi kutoka vyuo vya kilimo wawe na wigo mpana wa kujiajiri kwa kuhakikisha karakana za utengenezaji wa vipuri mbalimbali ambazo zipo katika vyuo vyetu na taaluma za utunzaji wa mazingira kwa kutengeneza mkaa mbadala iwe ni chachu kwa wahitimu kuweza kujiajiri “alisema Bw. Kusaya

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema chuo kishirikiane na viwanda vya sukari na wadau wengine katika kutatua tatizo la upungufu wa sukari nchini ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara hapa nchini.

“Tuandae mkutano utakaojumuisha Chuo Cha  Sukari Cha Taifa ,wadau wa uzalishaji wa sukari na wataalam  wengine ili kuhakikisha tatizo hili limekwisha” alisema Katibu Mkuu

Katibu Mkuu amemtaka Mkuu wa Chuo hicho Eng. Julius Deteba kuandaa andiko litakalo onesha mahitaji muhimu ili wizara iweze kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundimbinu na majengo ya chuo hicho.

Aidha, Katibu Mkuu ameshauri chuo hicho kushirikiana na wadau ili kupata eneo litakalotumika kuanziasha shamba darala la kilimo cha miwa.

Akihitimisha kikao chake na watumishi wa chuo hicho, amevitaka vyuo vya kilimo kujiendesha kibiashara ili kuweza kutatua changamoto zinazozikumba Taasisi hizo.