Skip to main content
Habari na Matukio

WADAU WA SEKTA YA MBEGU WAHIMIZWA KUWEKEZA ZAIDI KUZALISHA MBEGU ZA MBOGAMBOGA HAPA NCHINI


 Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi  Mhe. Charles John Tizeba, amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikisha Wadau wa Tasnia ya Mbegu kuandaa mkakati wa kusaidia uzalishaji wa kutosha wa mbegu  za mazao ya  mbogamboga.  Amesema hayo katika Warsha ya Wadau wa Mbegu iliyofanyika  katika Hoteli ya Mount Meru Arusha. 
Mhe. Waziri amesema, nchi kwa sasa inaupungufu mkubwa wa mbegu za mbogamboga ingawa uzalishaji wa mazao hayo umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa katika Uchumi na pato la Taifa.
Amesema, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Sheria ya Mbegu Na.18 ya Mwaka 2003 imefanya maboresho makubwa ya kuwezesha mbegu za Kilimo kupatikana kwa wingi hapa nchini. Kupitia marekebisho ya Sheria na Kanuni, kwa sasa, muda wa majaribio ya mbegu mpya umepunguzwa kutoka miaka mitatu na sasa majaribio hayo ni msimu mmoja tu hususan kwa mbegu zinazotoka nchi zenye makubaliano ya udhibiti wa Ubora wa mbegu na Tanzania ikiwemo nchi za SADC.
Aidha , Mhe. Waziri ameiagiza Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu nchini (TOSCI) kusimamia kwa karibu Sheria ya Mbegu ili kusaidia kuwalinda wakulima dhidi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wanauza mbegu zisizo na ubora  (Mbegu feki). 
Awali, aliwaeleza Wadau wa Mbegu nchini kuwa nchi ina  upungufu wa mbegu bora kutokana na uwekezaji mdogo kwenye tasnia ya Mbegu.
Aliwajulisha Wadau kuwa ili kuwezesha sekta binafsi kuzalisha mbegu zilizogunduliwa na vituo vya Utafiti vya Serikali, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imetoa Waraka maalumu unaoweka utaratibu wa jinsi ya sekta binafsi itakavyoweza kupata kibali cha kutumia mbegu hizo za umma. 
Amewaahidi Wadau kuimarisha Maabara ya Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) ili iweze kutekeleza vyema mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu masuala ya ubora  wa mbegu. Alisema, Wizara itatoa kiasi cha Dola za Kimarekani  13,000 kwa ajili ya kuwezesha Maabara ya TOSCI kupata ithibati (accreditation) ya Shirika la Kimataifa la Mbegu (ISTA). Ithibati hiyo itasaidia mbegu zinazozalishwa nchini ziweze kuuzwa bila kikwazo nje ya Tanzania.
Amewataka Wadau wa Mbegu kutumia fursa ya ardhi yenye rutuba kuanzisha na kuendeleza mashamba ya mbegu. Pia, aliwaasa washirikiane na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ili kupata maeneo ya kuzalisha mbegu kwa makubaliano maalumu.
Ameongelea fursa kubwa iliyopo kwenye kilimo kwa kuondolewa kwa tozo kwenye maeneo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo. Alisema, takriban tozo 80 zimeondolewa kwa Wizara ya Kilimo tu ukiondoa zile zilizokuwa zikisimamiwa na Wizara nyingine.
Aliwapongeza wafanyabishara wa mbegu kwa kuwa kiungo muhimu kwenye maendeleo ya tasnia ya mbegu. Aliahidi Wizara yake kuyafanyia Kazi yale ambayo yataazimiwa na Wadau wa mbegu.