Skip to main content
Habari na Matukio

Wadau Wakutana Kujadili Rasmu ya Mkakati wa Kuzuia Upotevu wa Chakula baada ya Kuvuna

Idara ya Usalama wa Chakula ya Wizara ya Kilimo leo wamekutana na wadau mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Morena iliyoko mjini Dodoma, lengo likiwa ni kupitia rasimu ya mkakati wa kuzuai upotevu wa chakula baada ya kuvuna.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa Warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Seushi Mburi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali  Watu amesema Mkakati huo utakapomalizika utakuwa na msaada mkubwa kwa wakulima kwani wamekuwa wakipoteza kiasi kikubwa cha chakula wakati wa kuvunwa na kuhifadhi.

Aidha Warsha hii itajadili namna ya kuzuia upotevu wa chakula baada ya kuvunwa kwa wakulima wadogo ambao wamekuwa wakipoteza zaidi ya asilimia 30-40 alisema Bwana Mburi.

Akitoa wito kwa wakulima na wadau wa kilimo Bwana Mburi amesema mkakati huu utakapo kamilika itakuwa fursa  kubwa kwa  wakulima katika kupambana na  hasara ambazo wamekuwa wakizipata.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama wa Chakula Bi. Josephine Amolo amesema Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha mazao hupotea baada na wakati  wa mavuno, hivyo Mkakati huo utawasaidia sana wadau hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye Clepin Josephat Mkemia Mkuu wa Wizara ya Kilimo amesisitiza kwamba ili nchi iweze kuwa na usalama wa chakula ni muhimu kuzuia upotevu wa chakula badala ya  wakulima  kusisitiziwa kuongeza eneo la uzalishaji wa chakula pekee.

"ili kuimarisha Usalama wa chakula ni vizuri kuzuia kilichopo kwanza kisipotee ndipo usalama wa chakula utaimarika' alisisitiza Clepin.

Anasema mkakati huu ulianza kwa kukusanya  maoni kutoka kwa wadua mbalimbali ambayo yanafanya mkakati huo kuwa shirikishi.

kwa upande wake Clara Melchior Msimamizi wa Miradi kutoka Ubalozi wa Swazland nchini Tanzania anasema nchi yake ina utaalamu mkubwa juu ya uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna hivyo kuamua kushirikiana na Tanzania ili kupunguza changamoto hiyo kwa wakulima hasa wadogo.

Pamoja na mambo mengine Bi Clara alisisitizia  wakulima kutumia mifuko maalum na vihenge vya chuma katika kuhifadhia  mazao baada ya kuvunwa ambayo imekuwa ikitolewa kwa gharama nafuu sana.