Skip to main content
Habari na Matukio

Wafanyabiashara Washiriki katika Kilimo – Komba

Mratibu wa Sera ya  Afya ya Udongo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo toka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bw. Canuth Komba ameitika sekta binafsi hapa nchini kushiriki kikamilifu katika kuinua kilimo.

Komba alitoa wito huu wakati wa mkutano wa Sera ya Afya ya Udongo  uliofanyika katika Hoteli ya LandMark Jijini Dar es Salaam, alisisitiza kuwa muda umefika kwa sekta binafsi kujikita kikamilifu katika kuboresha kilimo kwa manufaa ya wakulima wetu.

“Serikali peke yake haiwezi kuinua kilimo chetu bila ushiriki wa sekta binafsi  kikamilifu na hasa kwa wafanyabiashara wetu ambao ni nguzo muhimu katika uhakika wa soko la mazao ya wakulima.” alisisitiza Bw. Komba.

Wafanyabiashara ni watu muhimu sana katika kulisukuma gurudumu la kuinua sekta ya kili mo, aliongeza Komba.

Pia alifahamisha kuwa utafiti  umefanyika kwa lengo la kuwashauri watunga sera wetu kuwa na sera ya matumizi bora na sahihi ya mbolea kwa wakulima.

Elimu kwa wadau wa kilimo juu ya matumizi sahihi ya mbolea ni muhimu sana katika kufikia lengo kubwa la kuongeza uzalishaji wa kilimo chetu.

Mkutano huo wa siku moja  pia uliwashirikisha wadau mbali mbali kutoka Wizara Kilimo Chakula na Ushirika, Sekta Binafsi, Wakulima, Wafanyabiashara, watalaamu toka chuo kikuu cha Sokoine na chuo kikuu cha Mzumbe na nje ya nchi.

Mada mbali mbali ziliwasilishwa katika mkutano huo zikiwa na lengo la kuendeleza kilimo  kwa maslahi ya wakulima na taifa kwa ujumla katika harakati za kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania na kukuza pato la taifa.