Skip to main content
Habari na Matukio

Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Songea yafanikiwa kununua shehena ya Mahindi tani elfu10

Meneja wa Wakala wa Taia Hifadhi ya Chakula Kanda ya Songea Bwana Majuto Chabruma amesema Kanda yake imefanikiwa kununua kiasi hicho cha mahindi kwa mafanikio makubwa na kwa kuongeza Wilaya ya Songea Vijijini iliongoza kwa kuwa na uzalishamji na ambapo Wakala ilinunua kiasi kikubwa cha shehena ya mahindi.

Afisa Ugavi wa Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Songea Bwana Mujib Rajab alisema kwa ujumla wakulima wa maeneo mengi ambayo Wakala Kanda ya Songea ilikuwa imefungua vituo vya ununuzi zaidi ya 20 wamekuwa wakifurahia namna Serikali inavyowawezesha wakulima kiuchumi kwa kununua mahindi yao.  

“Kwa sehemu kubwa ya maeneo ambayo tuliweka vituo vya ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima, NFRA imekuwa ndiyo mkombozi, kwanza kwa kuwapa bei nzuri na ya uhakika lakini pia kuwalipa wakulima ndani ya muda, kwa kweli wakulima wengi wanaifurahia huduma zetu”. Amekaririwa Bwana Mujib.

Akizungumzi kuhusu ubora na usafi wa mahindi, Bwana Mujib Rajab amesema, wakulima wa Mkoa wa Ruvuma, wamekuwa na mwamko mkubwa wa kulima na kuzalisha mahindi yenye ubora na yaliyohifadhiwa katika hali ya usafi, na kuongeza kuwa, kumekuwa na changamoto kidogo katika Vituo vichache vya ununuzi lakini kwa sehemu kubwa ya mahindi yaliyonunuliwa na Wakala yalikuwa kwenye hali nzuri tofauti na awali.

“Mwaka huu hali ya ubora na usai ilikuwa ya kuridhisha na Wakala Kanda ya Songea imenunua mahindi mazuri na masafi, naweza kusema ni zaidi ya asilimia 98 kati ya shehena ya mahindi yaliyonunuliwa yalikuwa kwenye ubora unaotakiwa”. Amenukuliwa Bwana Mujib Rajab.

Naye Mhasibu wa Kanda Songea Bwana Ramadhan Nondo alisema bado kuna nafasi nzuri ya wakulima wa Mkoa wa Ruvuma na Mikoa jirani kuendelea kufurahia fursa ya kuuza mazao yao hususan mahindi kwa kuwa Kanda ipo kwenye mkakati wa kuongeza sehemu ya maghala yake.

Kwa sasa Wakala Kanda ya Songea itaanza ujenzi wa ghala dogo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 za nafaka lakini pia ikumbukwe kuwa Serikali iliamua kuja na mpango wa kujenga maghala makubwa na ya kisasa (Silos) ambapo Mkandarasi alishapatikana na ujenzi unataraji kuanza.” Amekaririwa Bwana Nondo.

Bwana Nondo aliongeza ujenzi huo si tu kuwa utabongeza uwezo wa Wakala Kanda ya Songea kuhifadhi nafaka zaidi ya tani elfu 29 za sasa lakini pia utaboresha mazingira na muonekano wa Ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Songea.

Bwana Nondo amekaririwa akisema “Bila shaka baada ya ujenzi kukamilika, Serikali itaongeza fedha zaidi za kununua mahindi kutoka kwa wakulima na hatutakuwa tena na changamoto ya mahali pa kuhifadhi na tutakuwa na nafasi nzuri ya kuwahudumia wakulima, na wananchi wenye mahitaji ya chakula ndani na nje ya nchi”