Skip to main content
Habari na Matukio

Wakulima katika Kanda ya Makambako waagizwa kuzingatia ubora na kuongeza thamani ya mazao yao

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako Bwana Bright Mollel alitoa ushauri huo kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini wakati wa mahojiano maalum.

Bwana Mollel aliwataka wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao kama wanataka kuendelea kulima kwa faida ili baadae iwe rahisi kwao kuuza mazao yao kama mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula au wanunuzi wengine.

Bwana Mollel amesema Wakala Kanda ya Makambako imekuwa ikiwaelimisha wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao hususan mahindi ili kuwasaidia yasikataliwe wakati wa msimu wa ununuzi unapoanza.

Bwana Mollel ameongeza kuwa Wakala imepewa dhamana na Serikali kununua mazao hususan mahindi hasa kwenye maeneo yenye ziada ya kutosha katika msimu wa mavuno lakini changamoto bado ipo kwenye ubora wa mazao.

“Naomba ikumbukwe na ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ununua mahindi kulingana na ubora wa bidhaa na kwamba mazao yanayonunuliwa na Wakala ni yale yenye kukidhi vigezo na lazima utaratibu huo tuusimamie” Amekaririwa Bwana Mollel.

Akiongelea hali hiyo, Msimamizi wa maghala ya Mbozi, Kituo kilichochini ya Wakala Kanda ya Makambako Bwana Elias Nicolaus alisema wakati wa msimu wa ununuzi unapofunguliwa mkulima anapoleta mahindi yake kwenye kituo cha ununuzi, atawakuta Watumishi wa Wakala ambao wamegawanyika kimamadaraka lakini kuna kuwa na mtu maalum ambaye kazi yake ni kuangalia ubora wa mahindi na usafi ukiwemo, na kama mahindi yanakuwa hayajafikia vigezo, uwa hayapokelewi.

Bwana Elias Nicolaus ameongeza kuwa changamoto hiyo ipo kwenye maeneo machache husuan kwenye Wilaya ya Ileje na kuongeza kuwa wameendelea kuwaelimisha wakulima kuzingatia ubora wa bidhaa kabla ya kuileta kwa  Wakala.

Tunaendelea kuwaelimisha wakulima na kuwafanya marafiki ili wawe na mazoea ya kupenda kutoa mazao bora na kwamba ukiwafanya wakulima kuwa marafiki mapema, unawasaidia kwanza kupenda kuzalisha kitu bora na kizuri lakini pia kuiona Taasisi (Wakala) kama sehemu yao”. Amekaririwa Bwana Elias Nicolaus.

Bwana Elias alitoa wito kwa wakulima kulima kwa lengo la kuzalisha bidhaa itakayouzika sokoni lakini pia amewaomba wafanyabiashara na wao kuhakikisha wananunua mazao kutoka tu kwa wale wakulima walizingatia vigezo vya ubora na usafi.

“Natoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wananunua mazao kwa kuzingatia ubora wa bidhaa na usafi lakini pia azma hii njema ya Serikali itafikiwa ikiwa tutaanzisha Mamlaka ya kudhibiti ubora kama ilivyokuwa kwenye Sekta ya Mafuta baada ya Mamlaka yenye Kudhibiti na Kusimamia Mafuta (EWURA) ilipoanzishwa”. Amekaririwa Bwana Elias Nicolaus. 

Kanda ya Makambako imekuwa ikihudumia Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe na jukumu lake kubwa ni kununua chakula cha ziada katika maeneo yaliyozalisha ziada kubwa na baadae kukihifadhi kwa ajili ya kusaidia wakati wa uhitaji. Katika msimu wa ununuzi wa 2016/2017 Kanda ya Makambako ilinunua kiasi cha tani elfu 16,279.298 za mahindi na kuyahifadhi kwenye maghala.