Skip to main content
Habari na Matukio

Wakulima Laki 5 Wapatiwa Mafunzo na Mradi wa EAAPP

Wakulima 599,290 kutoka Wilaya 48 hapa nchini, wamepatiwa mafunzo ya kilimo bora na mbinu za ujasiriamali katika kilimo kupitia Mradi wa EAAPP ulionza kutekelezwa mwaka 2010 hadi sasa. Hayo yamebainishwa na Afisa Kilimo Mkuu Bi. Justa Katunzi alipoongea na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ofisini kwake. Aliongeza kuwa wakulima wawezeshaji 2,414 na Maafisa Ugani, wapatao 697 nao walipatiwa mafunzo ili wasaidie wakulima katika maeneo wanayotoka.

Mafunzo hayo yalihusisha matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo kama mbolea, mbegu bora na matumizi ya madawa ya kuua wadudu, mafunzo hayo yalikuwa yakitolewa kwa njia ya mfumo wa shamba darasa ambapo wakulima wawezeshaji na wataalam wanafundisha wakulima kwa vitendo.

Mafunzo hayo yamewafanya  wakulima kuzingatia kanuni za kilimo cha kisasa hali ambayo imechangia matumizi ya mbegu bora kufikia  asilimia 90 katika maeneo yaliyofikiwa na mradi wa EAAPP.  
.
Aidha, Bi. Katunzi aliongeza kuwa mafunzo hayo yamewezesha wakulima kutoka Wilaya za Mbarali, Kilombero na Mvomero wanaotumia kilimo cha umwagiliaji kuongeza uzalishaji kutoka tani 2.5 na kufikia tani 8 kwa hekta na Wilaya ya Ukerewe inayotegemea mvua katika kilimo cha mpunga mavuno yamefikia 3.4 kutoka 1.5 kwa hekta.“Mafunzo ya ujasiriamali katika kilimo  yanayotolewa kupitia Mradi wa EAAPP yamewezesha wakulima kuongeza kipato kwa kuepuka hasara walizokuwa wakipata kutoka kwa walanguzi waliokuwa wakitumia vipimo visivyo rasmi kama vile lumbesa kuwadhulumu wakulima” Bi. Katunzi alifahamisha katika mazungumzo yake.

Alibainisha pia kuwa kabla ya mafunzo hayo, wakulima walikuwa wakiibiwa mazao yao kwa kutumia rumbesa, walikuwa wakiuza kilo 120  za mpunga kwa sh. 70,000 wakati kipimo halali ni kilo 100. Mafunzo hayo ya ujasiriamali, yamewawezesha wakulima kujua gharama walizotumia toka kuandaa mashamba,  kupanda na kuvuna hali ambayo imewawezesha kupanga bei ya kuuzia mazao kulingana na gharama za uzalishaji na bei ya soko. Mradi wa EAAPP ulianza  kutekelezwa mwaka 2010 na utakamilika mwezi Desemba, 2015.