Skip to main content
Habari na Matukio

Wakulima na Wafanyabiashara Kuhudhuria Maonesho ya Kilimo Sudani ya Kusini

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imepeleka wakulima na wafanya biashara wa mazao ya kilimo wapatao 14 katika ziara ya mafunzo katika nchi ya Sudani Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Eng. Christopher Chiza alisema hatua hiyo imekuja baada ya kupata mualiko kutoka kwa Waziri wa Kilimo wa nchini Sudan Kusini walipokuwa katika mkutano wa Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani (Agra) uliofanyika mjini Arusha.

 “Tumewateua ninyi muwe mabalozi wetu huko Sudan Kusini ili mtakaporejea muweze kuwafikishia wakulima wetu yale mtakayojifunza huko, pia muainishe mazao ambayo yana masoko kwa wingi nchini Sudan.”alisema waziri.

Waziri alisema kuwa mazao mengi ya Tanzania yamekuwa yakipatikana nchini Sudan kama vitunguu, na mchele  kwa bei ya juu lakini mkulima wa Tanzania  anakuwa hafaidiki hivyo kuwataka kuainisha fursa za masoko ili kuongeza kipato.

Waziri aliwahimiza wakulima na wafanyabiashara hao kuainisha fursa mbalimbali ambazo wakulima wa Tanzania wanaweza kunufaika nazo.

Wakulima kwa upande wao wameishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo muhimu ambayo itawawezesha kujifunza na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa wakulima nchini na kuwa chachu ya mabadiliko pindi watakaporejea.

Wakulima na wafanyabiashara wametakiwa kuangalia uwezekano wa kuongeza tija katika mazao kwa kusindika mazao na kuweka nembo ya Tanzania. Aidha, wakulima wametakiwa kutokuuza mazao mashambani kiholela bali wavune na kuyaongezea thamani.

Naye mkuu wa msafara huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Eng.  Mbogo Futakamba alisema wakulima na wafanyabiashara hao watapata nafasi ya  kuangalia na kujifunza  vikwazo vya kibiashara vilivyopo nchini Sudan ya Kusini ili kuweza kuvifanyia kazi watakaporejea nchini ili kurahisisha ufanyaji biashara nchini humo.

“Ziara hii ya mafunzo itawapa fursa wafanyabiashara na wakulima kujifunza uendeshaji biashara na pia watahudhuria maonesho ya wakulima” aliongeza  Futakamba.

Msafara huu pia utajumuisha wakuu wa wilaya ya Bahi Betty Mkwasa na wilaya ya Kakonko Ndugu Peter Toima  Kiroya na  utaongozwa na Naibu katibu Mkuu toka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Eng. Mbogo Futakamba, ziara hiyo ni  ya siku tano.