Skip to main content
Habari na Matukio

Wakulima Watakiwa Kuunda Umoja ili Kukabiliana na Soko

Wakulima wa viungo   Wilaya ya Muheza wametakiwa kutengeneza umoja wa wakulima wa mazao hayo  ili waweze kuwa na lugha moja katika kufanya biashara yao

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na  mataalamu wa mazao ya bustani kutoka Wizara ya Kilimo Idara ya uendelezaji wa mazao Bi Tabu Likoko baada ya kuwatembelea wakulima wa karafuu,tangawizi,pilipili manga iliki ,mdalasini na chai katika vijiji vya Mbomole,Amani na Hemsambia vilivyopo wilayani Muheza.

Akitolea mfano wa mazao ya korosho na pamba kwamba yameendelea kwa kasi kwa sababu yana usimamizi na chombo kinachosimamia maslahi yake, Bi Tabu amesema  umoja wa wakulima ndio chombo muhimu kitakachoweza  kusimamia wakulima ili kupata soko na ubora wa mazao.

Aidha aliwataka Wakulima wajiunge katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika katika maeneo yao ili kuanzisha mfumo wa stakabdhi ghalini ambao unamfanya mkulima kusubiri bei nzuri ya mazao ndipo wauze bizaa hiyo, alisema Tabu.

Naye Nasoro Bakari Kimangani mkulima wa mazao ya viungo ameiomba serikali kuharakisha  utaratibu huo ili mazao hayo yaweze kuwapatia wakulima faida na kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Aidha wakulima hao wanasema uzalishaji wa mazao ya viungo umeongezeka mara dufu lakini soko la uhakika bado ni changamoto kwao

Aidha ziara hii ya wataalamu kutoka Idara ya uendelezaji wa mazao ya kilimo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini imelenga kuimarisha mazao ya viungo hapa nchini pamoja na kutambulisha mazao hayo kwa jamii kuwa yanauwezo  mkubwa kustawi katika maeneo mengi ya Tanzania bara na kuliingizia taifa fedha za kigeni  alisistiza Bi Tabu.