Skip to main content
Habari na Matukio

Wakuu wa Wilaya Watakiwa Kutenga Ardhi kwa Vijana

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Eng. Christopher Chiza amewaagiza Wakuu wa Wilaya kote  nchini kutenga ardhi ya kilimo kwa ajili ya vijana. 

Mhe. Eng. Chiza ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa sherehe za maonesho ya Nane Nane  katika viwanja vya Nzuguni mjini Dodoma. 

Kufuatia agizo hilo  Wakuu wa Wilaya wa mikoa ya Dodoma na Singida kila moja alieleza jinsi gani ametenga ardhi ya kilimo kwa vijana katika wilaya yake. 

Aidha, Mhe.Eng. Chiza, ametoa wito kwa vijana kujikita kwenye kilimo kwakuwa ni ajira nzuri inayoweza kuwainua kiuchumi na kuongeza kipato.

Akielezea mpango wa serikali kuwekeza kwenye kilimo kwa vijana,  amesema hivi sasa kuna vijana wengi waliomaliza  vyuo wamejikita kwenye kilimo na serikali imewasaidia kuwapatia ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na  vijana hao wamekuwa ni mfano wa kuigwa na jamii nzima. 

Pia aliwafahamisha vijana na wakulima kuwa kuna uhakika wa  soko la mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi  katika nchi ya Sudani Kusini kwa sasa.

“Mazao mengi yanayotoka Tanzania yanapendwa na watu wa Sudani Kusini” alisema Mhe.Chiza
Aidha  amewataka wakulima kuchangamkia fursa ya soko hili ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufungashaji pamoja na uhifadhi wa mazao ili kuyaongezea thamani aliendelea kusema  Mhe. Chiza .

“Changamoto kubwa katika kilimo ni upatikanaji wa masoko pamoja na usindiksaji wa mazao, wakulima wakiweza kuhifadhi  na kusindika mazao vizuri wataweza kuongeza ushindani na nchi za jirani ikiwemo Kenya ambayo inachukua mazao Tanzania na kuifunga upya hivyo kuonekana kama yanatoka kwao”,alisema Mhe. Chiza.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Eng. Mbogo Futakamba, ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa ziara ya wakulima huko Sudani Kusini alielezea uhakika wa hali ya soko la mazao kuwa ni  mkubwa.
 Eng. Mbogo ameiomba serikali kufungua ubalozi wa Tanzania nchini humo ili wafanyabiashara wa kitanzania waweze kufanya biashara  kwa uhuru.

“Soko la bidhaa za kilimo nchini sudani ya kusini ni kubwa ili kutengeneza mazingira mazuri ya ki biashara ni vizuri serikali ya Tanzania ikaanzisha ubalozi wake humo, kwani wenzetu Kenya tayari wanaubalozi wao”,  alisema Eng.Mbogo