Wasanii walivyonogesha AGRF 2023 kwa burudani safi
Na Evance Ng'ingo
Kama ambavyo imezoeleka kwenye dhifa mbalimbali za kitaifa suala la burudani limekuwa ni chachu kubwa katika kuhakikisha washiriki wanaburudika na kufuatilia kwa umakini suala linalojadiliwa mbele yao.
Katika kongamano la kujadili mifumo ya chakula lililoanza Septemba 4 na linatarajia kumalizika leo Septemba 8, burudani imekuwa ni kiungo kikubwa katika kuhakikisha washiriki wa kongamano hilo wanafurahia siku hizo nne kwenye kongamano.
Burudani kwenye AGRF imegawanyika katika makundi mawili ambapo kuna upande wa kwenye bustani mahala ambapo wasanii Barnaba Elias, Khadija Kopa, Mzee Yusuph na Luby walikuwa wakitoa burudani safi kwa wageni.
Kwenye ukumbi ambapo mkutano ulikuwa ukiendelea kwa nyakati tofauti burudani ilitolewa na mwimbaji Angel Magoti, Jackson Mpanduka na pia liliimba kundi la Black Point la vijana saba.
Burudani ya Angel Magoti
Mwimbaji huyu wa nyimbo za Injili nchini, Angel Magoti alikuwa wa kwanza kufungua pazia la burudani siku ya tatu ya kongamano hilo siku ambayo Rais Dk Samia Suluhu Hassan alihutubia mbele ya marais na wageni wengine wakubwa.
Angel alizikonga haswa nyoyo kupitia wimbo wake wa Tupo Tayari ambapo amewahakikishia mataifa kuwa vijana wapo tayari kuleta mapinduzi ya kilimo.
Baada ya kuimba wimbo huo akiwa anashuka kutoka jukwaani Rais Samia Suluhu Hassan alishindwa kujizuia na kumkumbatia kwa furaha mwimbaji huyo.
Jackson Mpanduka
Huyu kama Angel yeye alipanda jukwaani kuimba peke yake wimbo wa kumpongeza Rais Samia ambapo aliimba kwa ufanisi wimbo huo na kutoa burudani safi.
Ulikuwa ni wimbo wa kupongeza harakati za Rais Samia katika kuendeleza kilimo na taifa kwa ujumla huku pia akipongeza harakati nzuri za Waziri wa Kilimo, Mh. Hussein Bashe za kusimamia sekta hiyo na yeye wimbo wake uliitwa Tuko Tayari.
The Bright Point
Hili kundi la vijana saba ambapo wao walikuwa na ujumbe mwanana wa kuelezea umuhimu, utayari na namna ambavyo wana imani na Rais Samia katika mapinduzi ya Kilimo.
Waliiambia dunia kuwa Tanzania inaweza na vijana wa Tanzania wanaweza kusababisha mapinduzi ya kilimo kupitia wimbo wao wa Africa Simama Walionesha uwezo wa kulimudu jukwaa kwa kuimba na uchezaji wao wao uliochagiza burudani safi.
Burudani wakati wa chakula cha mchana
Katika eneo la kulia chakula lililopo mkabala na Uwanja wa Gymkhana kulikuwa na burudani kabambe kutoka kwa wasanii ambapo walikuwa wakiimba live music chini ya jukwaa la kisasa lilifungwa na kampuni ya Peramiho Events
Msanii Elias Barnaba.
Msanii huyu alikuwa akiimba kwa umakini nyimbo zake na zingine za wasanii wa ndani na nje ya nchi.
Alikuwa na bendi yake ambapo alisifiwa kwa uwezo wake wa kutoa burudani laini kabla ya kupanda msanii mwengine Luby ambaye naye alikuwa wa moto sana katika burudani.
Khadija Kopa, Mzee Yusuph
Mwimbaji Khadija Kopa na Mzee Yusuph waliiwakirisha vema taarabu ambapo ilifikia wakati baadhi ya wageni baada ya kula walibakia wakicheza muziki kutoka kwa wasanii hao.