Skip to main content
Habari na Matukio

Wataalam Wakutana Kujadili Namna ya Kupata Takwimu Sahihi za Kilimo

Wadau wa CAADP  kutoka  Wizara ya Kilimo,   Viwanda na Biashara, Wizara ya  Mifugo na Uvuvi,  TADB, ANSAF ,NBS na SAGCOT wamekutana kujadili namna ya kupata takwimu halisi za kilimo nchi nzima.

Akizungumza na wataalam  hao katika Kikao kilifanyika  tarehe 24-25/01/2019  katika ukumbi  wa   Senate, Jengo  la Utawala  Chuo  Kikuu  Dodoma Bi. Jackline Mbuya ambaye ni Afisa Kilimo Mkuu  amesema kwamba upatikanaji wa takwimu za uhakika utasaidia kuimarisha sekta ya kilimo

Aidha Bi. Jackline amesema kwamba mpango wa kuwa na takwimu za uhakika ni mmuendelezo wa malengo waliyojiwekea  ikiwa  ni pamoja na kufufua na kuendeleza  Kilimo  barani Afrika  kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa njia endelevu ili kukifanya kilimo kikue kwa asilimia 6 kwa mwaka .

Bi. Jackline amesisitiza kwamba matokeo ya kikao kazi hicho yatasidia taifa katika upatikanaji wa chakula, kuleta maendeleo vijijini na kuondoa umaskini kwa   kujikita katika Nyanja za Uchumi, Siasa na Jamii.

Awali Bi. Jackline alibainisha kwamba Mpango  wa  Kuendeleza   Kilimo  barani Afrika  (Comprehensive Africa Agriculture Development  Programme  CAADP) uliandaliwa na kuridhiwa na baraza la Mawaziri wa Kilimo.

Katika mkutano huo wa wakuu wa nchi uliofanyika   Julai 2003  Maputo Msumbiji  waliazimia kutekeleza  yatokanayo na maamuzi husika na walipitisha Azimio  la  kutenga asilimia 10 ya bajeti za Serikali zao kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.

 Kutokana na kikao hicho wataalam wametakiwa kuwa na takwimu halisi za ukuaji wa  Kilimo ili ziweze kujazwa  na  kuwasilishwa  kwa matumizi  zikiwa ni takwimu za Kilimo za  nchi nzima.