Wataalamu wa Kilimo Wametakiwa kutafuta suluhisho la changamoto ya masoko ya mazao ya kilimo
Wataalamu wa Kilimo wametakiwa kutafuta suluhisho la changamoto ya masoko ya mazao ya kilimo badala ya kusisitiza uongezaji wa uzalishaji pekee.
Akizungumza na wataalamu wa Wizara ya Kilimo hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo Naibu Waziri Mhe. Omari Mgumba amewataka wataalamu kusisitiza Kilimo cha Kibiashara ambacho mkulima anazalisha kulingana na mahitaji ya soko.
Aidha, amesema wakulima wamekuwa na mwitikio mkubwa sana katika uzalishaji wa mazao mbalimbali lakini wamekuwa wakikosa soko hivyo kushindwa kuendelea na uzalishaji kwa kuona kama kilimo hakilipi.
Akitolea mfano wa zao la mbaazi alisema mwaka jana Wizara ilihamasisha wakulima kulima mbaazi kwa wingi bila kuangalia mahitaji ya bidhaa hiyo kwenye masoko ya kimataifa jambo ambao lilisababisha wakulima kukaa ndani na bidhaa zao hivyo ni muhimu uhamasishaji wa uzalishaji uendani pamoja na utafutaji wa masoko alisisitiza Mhe. Mgumba.
"Nataka tuwatembelee wanuuzi wa mbaazi na mazao yanayofanana ili kujua namna ya kuimarisha soko la bidhaa hiyo", alisema Naibu Waziri.
Hata hivyo amewataka wataalamu hao kuacha siasa na kufanya kazi zao kitaalamu ikiwa ni pamoja na kuwashauri viongozi vizuri ili kuweza kufikisha lengo la uwepo wa Wizara ya Kilimo kwa wananchi ambao kilimo ni sehemu ya maisha yao.
Aidha, amewataka wataalamu wa Utafiti wa Kilimo kuja na mkakati ambao utasababisha pamba iweze kutumika zaidi hapa nchini badala ya kusafirishwa nje.
Awali ya hapo Naibu Waziri alisema kwamba asilimia 70 ya pamba yote inayolimwa hapa nchini inasafirishwa nje ya nchi na asilimia 30 tu ndiyo inayobaki hapa nchini kwa ajili ya matumizi mbalimbali alisisitiza.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akihitimisha mkutano huo amesema kwamba Wizara kwa sasa inatoa mafunzo kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya kuendeleza zao la mpunga na tija (ERPP) Kuhakikisha uzalishaji kwa ekari unaongezeka kutoka gunia tano (5) hadi kumi na mbili (12) kwa ekari mpaka gunia 40 hadi 45.
Amesema ongezeko la uzalishaji huo umeonekana katika maeneo mengi ambayo Mradi huo umekuwa ukitekelezwa ikiwemo katika Wilaya saba (7) za Mkoa wa Morogoro ambapo wakulima wengi sasa huvuna kuanzia gunia 35 hadi 45 za mpunga .
Hata hivyo Mhandisi Mtigumwe amesema Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili iliyozinduliwa mwanzoni mwa mwezi June mwaka huu inasimamia uzalishaji wenye tija na faida katika Sekta za Kilimo alisisitiza.
Akizungumzia masoko Katibu Mkuu amesema kwamba Muundo Mpya wa Wizara kwa sasa unakuwa na Kitengo cha Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agriculture Marketing ) hivyo kitakuwa ni suluhisho kubwa kwa masoko ya mazao ya kilimo.
"Mwanzoni tulikuwa tunahamasiha uzalishaji wa mazao tukiamini wenzetu wa Viwanda wanashughulikia masoko ya mazao ya wakulima wetu lakini kwa sasa kwa kuanzishwa Kitengo hicho ni dhahiri kwamba tatizo la masoko limepata dawa" .alisema Katibu Mkuu.
Hata hivyo Vyuo vya Kilimo pamoja na kubadilishwa mitaala lakini pia vitatumika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa Maafisa Ugani waliopo na wanaojiriwa ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya kilimo na teknolojia mbalimbali, alimalizia Mhandisi Mtigumwe.
Mwisho.