Skip to main content
Habari na Matukio

WATUMISHI SEKTA YA KILIMO FANYENI KAZI KWA KUJIAMINI-KM KUSAYA

Muheza

Watumishi wa Sekta ya Kilimo nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kujiamini na weledi ili kuongeza tija katika kuhudumia wakulima na  hivyo kufanya Sekta ya Kilimo iwe na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo (27.04.2020) wilayani Muheza mkoa wa Tanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipoongea na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano na wale wa Chuo cha Mafunzo  Kilimo (MATI) Mlingano.

“ Watumishi msijione wanyonge kwenye shughuli zenu, nataka mjiamini na muwe wabunifu katika kutekeleza kazi za wananchi ili tija iongezeke kwa Wizara na Taasisi zake kutoa huduma bora “ alisema Kusaya

Kusaya alisema ni wakati muafaka sasa watafiti wa zao la mkonge kujikita katika kutoa matokeo chanya ya mbegu kwani kuna maeneo mengi nchini kama wilaya za Kahama, Kishapu, Kilosa na Geita wameonesha nia ya kuanzisha mashamba ya zao la mkonge.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kituo cha TARI Mlingano , Mkuu wa kituo hicho Dkt.Catherine Senkoro  alisema uzalishaji wa mbegu mpya za mkonge zenye uwezo mkubwa wa mavuno  umefikia mbegu 500,000 kati mahitaji ya wakulima ya mbegu 1,600,000 kwa mwaka.

Dkt.Senkoro alisema kwa sasa wana mkakati wa kuzalisha mbegu bora za mkonge kwa kutumia teknolojia ya maabara na vipando ili kuweza kufikia lengo la kuzalisha mbegu 2,000,000 ifikiapo mwaka 2021.

Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu aliagiza taasisi ya TARI Mlingano kuhakikisha inazalisha mbegu 5,000,000 kwa mwaka na kuwa Wizara yake itatoa fedha za kuwezesha utafiti na uboreshaji maabara ya kupima afya ya udongo na ile ya kuzalisha mbegu bora za mkonge.

“Wizara ya Kilimo ipo tayari kusaidia kituo hiki kupata fedha za kutosha ili kuzalisha mbegu bora za mkonge na kuwafikia wakulima wengi zaidi kama alivyoagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipotembelea kituo hiki Machi mwaka huu” alisema Kusaya

Kwa mujibu wa Dkt.Senkoro kwa sasa ekari moja inazalisha tani moja ya mkonge wakati China wanazalisha tani tano kwa ekari na kusema taasisi hiyo inahitaji kuongezewa nguvu ili izalishe mbegu bora zenye kutoa matokeo makubwa kwa wakulima.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alitembelea na kuongea na watumishi wa Vyuo vya mafunzo ya Kilimo  ambapo aliwataka wawe watulivu wakati serikali ikifanya maboresho na  ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho.

Kusaya aliwakumbusha watumishi hao kuwa kazi ya ualimu ni ya wito hivyo wasichoke  badala yake waifanye kwa moyo na jitihada kufundisha vijana na wakulima mbinu bora za kilimo.

Katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na weledi wa kazi,Katibu mkuu Kusaya amewataka watumishi kujitokeza na kuomba nafasi ya kwenda masomoni kujiendeleza kielimu na kuwa serikali itawezesha .

“Katika kipindi hiki nataka watumishi wa wizara ya Kilimo na taasisi waweze kujiendeleza kwa mafunzo ya muda mrefu  au mfupi ili wasaidie serikali kuboresha utoaji huduma na tija katika usimamizi wa sekta ya kilimo nchini .” alisisitiza Kusaya

Nao watumishi  Mary Zakayo na Valentine Njau wa chuo cha MATI Mlingano walimuomba Katibu Mkuu asaidie waweze kupata stahili zao za malipo ya likizo na madeni ya vibarua.

Akijibu maombi hayo ,Kusaya alisema kuanzia mwezi  ujao Mei watumishi hao watalipwa madeni yao kwani Wizara imepokea tayari shilingi Bilioni Tano kulipa madeni ya watumishi na watoa huduma kwa taasisi zote chini ya Wizara ya Kilimo..

Mwisho

Imetolewa na ;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

TANGA

27.04.2020