Skip to main content
Habari na Matukio

WATUMISHI WAPYA KILIMO WAPIGWA MSASA KUHUSU MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Jumla ya Watumishi 36 wa Wizara ya Kilimo Makao Makuu leo tarehe 4 Februari, 2021 wameanza kupata mafunzo yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu maadili ya utumishi wa umma pamoja na utoaji wa huduma kwa umma.

Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili kwa niaba ya Katibu Mkuu; Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Philbert Lutale amesema mafunzo hayo ambayo Wizara imeyatoa kwa Watumishi wapya yanalengo la kuwaanda Watumishi hao kwenda sambamba na mahitaji ya nyakati pamoja na mahitaji ya Wateja (Wakulima na Wadau wa Sekta ya Kilimo Mazao) nchini kote.

Kaimu Mkurugenzi Lutale ameongeza kuwa utoaji wa huduma kwa Wananchi walio kwenye Sekta ya Kilimo Mazao unaongozwa na Dira ya Wizara ambayo inasema: - Wizara itakuwa kiini cha kutoa mwongozo wa sera na huduma kwa kilimo cha kisasa na chenye tija faida na ushindani kibiashara ili kuimarisha ustawi wa Wananchi, usalama wa chakula na lishe.

Bwana Lutale amewaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa Wizara inawatarajia baada ya mafunzo hayo watakuwa mahili kwenye maeneo ya maadili ya utumishi wa umma; Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma; utunzaji wa kumbukumbu na taratibu za ofisi.

Eneo lingine ni pamoja na kujua muundo wa Serikali na uendeshaji wa shughuli zake pamoja na kufanyiwa upekuzi (Security vetting) kwa mujibu wa taratibu za Serikali.

Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Lutale amemalizia kwa kutoa wito kwa Watumishi hao waliopata fursa hiyo kuwa Taifa linawataraji na kwamba wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu.

“Fanyeni kazi zenu kwa bidii kwa moyo na pendeni na kufurahia kwa kufanya hivyo, mtakuwa mkijitofautisha kwa kuwa kila anayefanya kwa bidii atapimwa kwa juhudi yake.

“Kila mmoja ana umuhimu katika eneo lake la kazi; Mfano Mwangalizi wa Ofisi, Dereva, Mhasibu au Mchumi. Mtumishi mmoja hasipofanya kwa sehemu yake katika wakati wake; Wote tutaathirika. Kama umepewa dhamani fulani basi ifanye kwa bidii na juhudi na kwa moyo wako wote.” Amekaririwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Philbert Lutale

Naye Margaret Ngondya kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa mafunzo hayo kwa Watumishi wake.

Margaret amesema Wizara ya Kilimo kama Taasisi ya Umma; Inatakiwa kuwa ikiandaa mafunzo kama hayo kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi kwa njia ya mafunzo ya mara kwa mara.

Margaret amesema Wizara na Taasisi za Umma zinaongozwa kwa Miongozo,Sheria, Kanuni na Taratibu hususan Sheria za Kisekta (Sekta ya Kilimo) Sheria ya Utumishi wa Umma; Kanuni za Utumishi wa Umma 2003; Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma 2005 na kuongeza kuwa ni vyema Watumishi Wapya na wa zamani wakawa wanakumbushwa mara kwa mara ili kuendelea kuwafanya kuwa bora na mahili katika utumishi wa umma.

Bi. Margaret ameongeza kuwa katika siku hizo mbili. Watumishi wa Wizara watajifunza kuhusu misingi ya maadili katika utumishi wa umma na kanuni zake nane (8) ambazo ni: - Kutoa Huduma Bora; Utii kwa serikali; Bidii ya kazi; Kutoa huduma bila upendeleo; Kufanya kazi kwa uadilifu; Kuwajibika kwa umma; Kuheshimu sharia na Matumizi sahihi ya taarifa.