Skip to main content
Habari na Matukio

WATUMISHI WIZARA YA KILIMO CHAPENI KAZI KWA WELEDI-KM KUSAYA

Menejimenti ya Wizara ya Kilimo imetakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi katika kutekeleza maagizo ya Rais kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa chakula.

Kauli hiyo imetolewa leo (24.03.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati wa hafla ya makabidhiano rasmi ya ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu Mhandisi Mathew Mtigumwe yaliyofanyika makao makuu ya wizara Mtumba mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya wizara.

Kusaya alisema wizara ya kilimo ina changamoto ya kuhakikisha watanzania wanakuwa na uhakika wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwa ubora.

“Kila mtumishi wa Wizara ya Kilimo ahakikishe anafanya kazi kwa bidii na weledi kutekeleza malengo yote tuliyowekewa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika na usalama wa chakula” alisema Katibu Mkuu Kusaya

Kusaya aliongeza kusema anamshukuru Mhandisi Mtigumwe kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa wizara ya kilimo wakati wa uongozi wake ikiwemo kupitia mabadiliko yaliyofanyika katika idara na taasisi.

Kwa upande wake Mhandisi Mtigumwe alisema anawashukuru watumishi wote wa wizara ya kilimo kwa ushikiano waliompa alipokuwa Katibu Mkuu na kwamba anajisikia vema kuona wizara na taasisi zake wanachapa kazi

Alitaja changamoto za sekta ya ushirika na umwagiliaji kuwa zinahitaji msukumo mkubwa ili taswira ya wizara ya kilimo iendelee kuwa nzuri.

“Ushirika bado ni changamoto,nawaachia japo tulianza mchakato wa maboresho ya sheria endeleeni ili wakulima wa Tanzania wanufaike na jasho lao “ alisema Mhadishi Mtigumwe ambaye kwa sasa amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu .

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Mkurugenzi wa Mipango Bora ya Ardhi ya Kilimo Paulo Tarimo alimshukuru Katibu Mkuu aliyepita Mhandisi Mtigumwe kwa ushirikiano na maelekezo aliyoyatoa wakati wa utumishi wake.

Mkurugenzi huyo ameahidi kwa niaba ya Menejimenti na watumishi wa wizara ya kilimo kutoa ushirikiano zaidi kwa Katibu Mkuu Kusaya ili malengo ya Taifa yafikiwe.

Mwisho

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

DODOMA