Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI BASHE AZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA WA SEKTA YA KILIMO

WAZIRI BASHE AZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA WA SEKTA YA KILIMO

Waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe, leo tarehe 5 Julai, 2022, amezindua kituo cha huduma kwa wateja wa Sekta ya Kilimo; Kituo kitakachotoa nafasi kwa Wakulima, Wauzaji wa pembejeo, na Watoa huduma wengine kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo kupiga simu bure ili kupata taarifa za kilimo na majibu ya kila changamoto wanayokutana nayo.

Bashe amesema, Wakulima na Wadau wengine watakuwa wakipiga simu hiyo ya namba ya bure ili kupata taarifa na kuuliza maswali yanayohusu Sekta ya Kilimo mazao, hali ya hewa, taarifa za matumizi ya mbolea, viuatilifu na masoko, lengo likiwa ni kuwafikia popote walipo.

Waziri Bashe amesema jambo hilo ni mwanzo wa kuelekea hatua kubwa ya mafanikio ambapo Wakulima watakuwa wakipata taarifa ya mazao gani yanatakiwa sokoni ili walime kwa wingi kulingana na mahitaji ya soko.

"Wakulima watakuwa wakipiga simu ya bure kwa namba ya huduma kwa wateja ambayo ni 0733800200 itakayomuunganisha moja kwa moja na Mtaalamu kutoka Wizara ya Kilimo”. Amesema Bashe.

Amefafanua kuwa, awali Watoa Huduma walikuwa wakisikiliza changamoto za Wakulima kwa njia ya simu kupitia ujumbe mfupi (Text msgs), lakini sasa watasikilizwa kwenye simu moja kwa moja na mfumo huo unatunza taarifa za Wateja; Ambapo kama swali la Mteja halijajibiwa muda huo, basi litajibiwa baadae.

Amesema kuwa baada ya mfumo wa huduma kwa Wateja kukamilika nchi nzima Kitengo cha Masoko kitakuwa kikitoa taarifa za bei za mazao sokoni, zinakwendaje.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde amesema kazi kubwa imefanyika ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wateja kwa njia mbalimbali.

Amesema mkakati uliopo ni kuanzisha channel maalum ya Televisheni ambayo itaonyesha maudhui ya kilimo kwa muda mferu.

Kwa upande wake; Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Andrew Massawe amesema, takwimu zinaonyesha mfumo wa M-Kilimo umesaidia kwa kiasi kikubwa Wakulima kupata taarifa za haraka, ambapo Wizara imefanikiwa kusajili Wakulima milioni 5.5 kupitia mfumo huo, wakati Watoa huduma kutoka nje, waliosajiliwa ni 3,905 ambapo takwimu zinaonyesha changamoto 60,120 za Wakulima zilitafutiwa majibu.

MWISHO!