Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI MKUU AFUNGUA SOKO LA MAZAO SONGEA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amefungua mradi wa maghala ya kuhifadhi nafaka na soko la mazao la OTC-Lilambo katika Halmashauri ya Songea uliogharimu sh. bilioni 1.5.

Amesema Rais Dkt. John Magufuli ameazimia kuwawezesha wakulima kuwa na mahala pa uhakika pa kuhifadhia mazao yao na sehemu ya kufanyia biashara ili kuwaongezea tija.

 

Amefungua soko hilo leo (Alhamisi,  Januari 3, 2019) akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Ruvuma.

 

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi wa soko hilo pamoja na maghala kwani umezingatia viwango. Maghala hayo mawili yana uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 za nafaka.

 

“Licha ya soko hili kuwapa wakulima wetu fursa ya kupata masoko ya kuuzia mazao yao, pia  watapata mafunzo ya namna ya kuhifadhi bidhaa zao pamoja na taarifa za masoko.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza bodi ya soko hilo kuhakikisha inatoa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari ili wakulima waweze kupeleka mazao yao sokoni hapo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha nchini kuandaa mashamba, kupanda mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

“Nawaagiza viongozi wa kata na vijiji hakikisheni wananchi katika maeneo yenu wanaandaa mashamba na kupanda kwa wakati, tunataka tuwe na chakula  cha kutosha na ziada tuuze.”

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Songea, Martin Mtani ameiomba Serikali iwapatie mashine itakayowawezesha kupanga madaraja ya mazao ya nafaka mbalimbali.

 

Mkurugenzi huyo ameomba soko hilo liwekwe kwenye mpango wa kujengewa vihenge vyenye uwezo wa kukausha mazao kwa viwango vya kimataifa ili kutatua tatizo la unyaufu.

 

Pia Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali iwasaidie katika kuliunganisha soko hilo na TMX ili waweze kuuza mazao ya nafaka ndani na nje ya nchi .

 

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga.


Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme na maafisa wengine wa Serikali.