Skip to main content
Habari na Matukio

Waziri Nchemba Afanya Mazungumzo na Balozi wa Ireland Nchini

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Lameck Chemba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bi. Fionnuala Gilsenan ofisini kwake katika jitihada zake za kuinua sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. 

Waziri Nchemba alimweleza Balozi huyo kuhusu hali ya sekta ya kilimo na mikakati ya serikali katika kukabiliana na changamoto zinazokikumba kilimo chetu hapa nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mbegu, ambapo vituo vya utafiti vya serikali na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) vimejikita katika kutafiti mbegu mbali mbali.

“Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima wetu” alieleza Mhe. Chemba.

Pia alisema kuwa uzalishaji wa mbegu bora na hasa za viazi utasukumwa kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ili ziweza kupatikana kwa wakati kwa wakulima wetu.

Upatikanaji wa uhakika na kwa wakati wa mbolea kwa wakulima ni moja ya mikakati ya Serikali katika kuboresha na kuinua kilimo.

Mikakati mingine kwa mujibu wa Waziri Nchemba ni kwa upande sekta ya mifugo ambapo kuna changamoto ya kuwabadilisha wafugaji kutoka ufugaji wa kiasili na kuingia katika ufugaji wa kisasa.

Jitihada nyingine ni kuwaingiza vijana katika ufugaji wa kisasa wa samaki kwa kuwawezesha kupata zana bora za uvuvi, alibainisha Mhe Nchemba.

Balozi Bi. Gilsenan alimfahamisha Waziri Nchemba kuwa nchi yake imedhamiria kusaidia kuinua tija kwa kuboresha mnyororo wa thamani ya mazao.

Sehemu nyingine muhimu kwa mujibu wa Bi. Gilsenan ni pamoja na huduma za ugani, hifadhi na matumizi bora ya ardhi yanayolenga kupunguza migogoro, na kuchochea upatikanaji wa masoko kwa mazao yanayozalishwa. 

Naye Mratibu wa Kitengo cha Mahusiano na Misaada ya Kimataifa kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Bi. Margareth Ndaba ameainisha maeneo ambayo Ireland inaweza kusaidia kuwa ni pamoja na lishe, Kilimo cha mboga mboga, zana za kilimo, utafiti na viwanda vya maziwa ili kusaidia kuondoa umaskini kwa Watanzania.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Mifugo , Tanzania Dkt. Furaha Mramba alianisha changamoto ambazo Ireland inaweza kusaidia katika kuendeleza mifugo kuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuibua magonjwa mapya ya mifugo.

“Tunaomba Ireland kusaidia katika chanjo za mifugo ili kupambambana na magonjwa yanayoambatana na mabadiliko ya tabianchi” , alisisitiza Dkt Mramba.

Wakati huo huo Waziri Nchemba alikutana na wadau wa kilimo cha viazi kutoka Finland wakiongozwa na Naibu Balozi wa Finland nchini, Bwana Simo – Pekka Parviainen ambapo walimweleza nia ya kutaka kujikita katika kuboresha kilimo cha viazi mviringo. 

Naye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Peruna Mestant Bwana Aero Pisila alimfahamisha Waziri kuwa tayari wametembelea Mkoa wa Mbeya, Njombe na Arusha ili kuona fursa ya kuinua kilimo cha viazi mviringo na hasa kwa vijana wa Tanzania. 

Aidha, Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza kilimo cha Viazi Mviringo hapa nchini Bi. Matilda Byanda alifamweleza Waziri kuwa tayari wamefanya ziara za kujitambulisha katika Mikoa husika na kuonana na viongozi wa serikali na watalaam wa kilimo katika ngazi za halmashauri na kanda husika.

Waziri Nchemba aliwataka kubainisha maeneo ambayo serikali itachangia katika kutimiza lengo hilo la kuboresha kilimo cha viazi mviringo.